Waislamu wahamakishwa na hatua ya Kosovo kufungua ubalozi Quds
(last modified Mon, 15 Mar 2021 10:50:06 GMT )
Mar 15, 2021 10:50 UTC
  • Waislamu wahamakishwa na hatua ya Kosovo kufungua ubalozi Quds

Waislamu wameghadhabishwa mno na kitendo cha Kosovo kufungua ubalozi wa nchi hiyo ndogo ya Ulaya katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.

Kosovo hapo jana Jumapili ilikuwa nchi ya kwanza ya Kiislamu kufungua ubalozi katika mji mtukufu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel, baada ya Tel Aviv kudai kuwa imeutambua uhuru wa taifa hilo. Ufunguzi huo unajiri baada ya kutiwa saini mapatano kati ya Kosovo na utawala wa kibaguzi wa Israel kwa ajili ya kufungua ubalozi wa nchi hiyo ya eneo la Balkan katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Wasel Abu Youssef, mjumbe wa Kamati Kuu ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) amesema hatua ya kufunguliwa ubalozi wa Kosovo huko Quds inayokaliwa kwa mabavu ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Waislamu katika mitandaoni ya kijamii wamesema ufunguzi huo wa ubalozi wa Kosovo katika mji wa Baitul-Muqaddas unalenga kuidhoofisha kadhia ya Palestina, ambalo ndilo suala kuu kwa ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa.

Maafisa wa serikali ya Uturuki wamesema viongozi wa Kosovo wamekanyaga maazimio ya kimataifa na kwamba walipaswa kujiepusha na hatua hiyo inayotoa pigo kwa hali na nafasi ya kihistoria na kisheria ya Quds.

Jamhuri ya Czech ilipofungua ubalozi wake Quds hivi karibuni

Haya yanajiri siku chache baada ya Jamhuri ya Czech kufungua ubalozi wake katika mji huo wa Baytul-Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.

Mbali na Kosovo na Czech, Guatemala pia imefuata kibubusa hatua ya Disemba mwaka 2017 ya aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump ya kuchukua uamuzi wa upande mmoja wa kuutambua mji mtakatifu wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, na kutangaza kuhamishia ubalozi wa Washington mjini humo kutoka Tel Aviv.