Hamas: Kutiwa nguvuni Wapalestina huko Saudia kunawanufaisha Wazayuni
(last modified Tue, 06 Apr 2021 02:47:44 GMT )
Apr 06, 2021 02:47 UTC
  • Hamas: Kutiwa nguvuni Wapalestina huko Saudia kunawanufaisha Wazayuni

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ametilia mkazo udharura wa kuachiwa huru makumi ya Wapalestina wanaoshikiliwa mahabusu nchini Saudi Arabia na kusema kuwa, kufungwa kwa Wapalestina hao huko Saudia kunawanufaisha Wazayuni wa Israel.

Hazim Qassem ameashiria suala la makumi ya Wapalestina wanaoshikiliwa mahabusu huko Saudi Arabia akiwemo mwakilishi wa zamani wa Hamas huko Riyadh na kusema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ndio peke yake unaonufaika na kuwekwa mahabusu Wapalestina hao huko Saudia. Amesema kuwa, kamata kamata hiyo ya Saudia inawalenga wanaharakati wa Kipalestina. 

Msemaji wa Hamas ameongeza kuwa, harakati hiyo inalaani kitendo cha Saudi Arabia cha kuendelea kuwashikilia mahabusu makumi ya Wapalestina waliotiwa nguvuni tangu miaka miwili iliyopita bila ya sababu yoyote ya kisheria, na wakati huo huo inatoa wito wa kuachia huru mara moja Wapalestina hao, kwa sababu hawajafanya kosa lolote na wanaishi nchini Saudi Arabia kwa njia halali. 

Familia za Wapalestina hao wanaoshikiliwa mahabusu huko Saudi Arabia zinasema, maafisa wa serikali ya Riyadh wamewatia nguvuni ndugu zao kwa sababu tu ya kuwa na uhusiano na harakati ya Hamas na mapambano ya ukombozi ya wananchi wa Palestina dhidi ya Israel. 

Msemaji wa Hamas amesema, harakati hiyo imefanya juhudi kubwa za kikanda na kimataifa ili kuhakikisha Wapalestina hao wanaoshikiliwa mahabusu nchini Saudi Arabia wanaachia huru lakini juhudi hizo zimeambulia patupu na Riyadh inaendelea kuwashikia raia hao kinyume cha sheria.   

Tags