Lebanon; nchi yenye mawaziri wakuu wawili kwa wakati mmoja
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i69404-lebanon_nchi_yenye_mawaziri_wakuu_wawili_kwa_wakati_mmoja
Katika miezi minane iliyopita, Lebanon imekuwa na mawaziri wakuu wawili kwa wakati mmoja. Tarehe 4 Agosti mwaka uliopita mji mkuu wa nchi hiyo Beirut, ulishuhudia mlipuko mkubwa ambao ulipelekea watu karibu 200 kupoteza maisha.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 24, 2021 22:08 UTC
  • Lebanon; nchi yenye mawaziri wakuu wawili kwa wakati mmoja

Katika miezi minane iliyopita, Lebanon imekuwa na mawaziri wakuu wawili kwa wakati mmoja. Tarehe 4 Agosti mwaka uliopita mji mkuu wa nchi hiyo Beirut, ulishuhudia mlipuko mkubwa ambao ulipelekea watu karibu 200 kupoteza maisha.

Licha ya kuwa kwa miezi saba wapinzani walikuwa wameshindwa kuiondoa madarakani serikali ya Waziri Mkuu Hassan Diab, lakini mlipuko huo uliwasaidia pakubwa na hatimaye kuwawezesha kumfukuza kazi.

Tokea Agosti mwaka uliopita, Lebanon imekuwa ikiendeshwa na serikali ya muda inayoongozwa na waziri mkuu huyo. Licha ya Mustafa Adib kutangaza kuwa hakuwa na uwezo wa kubuni serikali ikiwa ni mwezi mmoja tu baada ya kupewa fursa hiyo, lakini katika upande wa pili Saad Hariri ambaye alichukua nafasi yake naye amekwamba na kushindwa kuunda serikali, lakini pamoja na hayo hataki kujiuzulu kama alivyofanya mwenzake aliyemtangulia.

Suala linaloonekana wazi siku hizi ni safari za mara kwa mara zinazofanywa nje ya nchi na Hassan Diab na  Saad Hariri. Hivi sasa Diab ni kiongozi rasmi wa Lebanon ambaye anasimamia serikali katika hali ambayo Hariri ambaye amepewa jukumu la kubuni serikali mpya hachukuliwi kuwa kiongozi rasmi wa nchi hiyo.

Hassan Diab

Hivi karibuni Hassan Diab alifanya safari Qatar ambapo alikutana na kufanya mazungumzo rasmi na viongozi wa nchi hiyo ndogo ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi. Walio karibu na serikali yake wanasema kwamba lengo la safari hiyo lilikuwa ni kuwaomba viongozi wa serikali ya Qatar waisaidie kifedha Lebanon kutatua matatizo yake ya kiuchumi.

Hariri naye katika miezi ya karibuni amefanya safari katika nchi za Imarati, Uturuki na hivi sasa Italia ambapo amekuwa akifuatilia malengo kadhaa, hasa ya kisiasa.

Lengo lake la kwanza ni kuyafahamisha makundi ya kisiasa ya Lebanon kwamba hayuko tayari kujiuzulu nafasi aliyopewa ya kuunda serikali mpya na kwamba bado ni shakhsia muhimu katika siasa za Lebanon ambaye anakubalika katika ngazi za kimataifa.

Lengo la pili la safari hizo ni kutuma ujumbe huu kwa jamii ya kimataifa kwamba Rais Michel Aoun wa nchi hiyo ndiye anayekwamisha juhudi za kubuniwa serikali mpya. Katika safari yake Italia, Hariri alimshambulia vikali kwa maneno Rais Aoun na kudai kuwa katika hali ambayo yeye Hariri amekuwa akifanya safari za nje kwa ajili ya kushughulikia majukumu rasmi ya kikazi na kwa madhumuni ya kuisadia Lebanon lakini baadhi ya watu katika ikulu ya Beirut wamekuwa wakifanya safari za nje kwa malengo ya kitalii tu. Matamshi hayo bila shaka yanabainisha kuwepo tofauti kubwa kati yake na Rais Aoun na pia yanaonyesha kutokuwepo mpango maalumu wa kubuniwa serikali mpya ya Lebanon hivi karibuni.

Lengo la tatu la safari za mara kwa mara za Hariri nje ya nchi ni kuwataka wachezaji muhimu katika siasa za Lebanon wazingatie zaidi mgogoro wa nchi hiyo kuhusiana na kubuniwa serikali mpya ya Beirut. Kupitia safari hizo Hariri anawataka washirika wake wa kigeni wamshinikize Aoun kwa maslahi yake ya kisiasa. Pamoja na hayo lakini matukio ya miezi sita iliyopita yanathibitisha wazi kwamba siasa hizo za Hariri zitafeli tu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba Michel Aoun anaendelea kushikilia msimamo wake na wala hayuko tayari kushinikizwa na nchi za nje.

Saad Hariri (kushoto) akiwa safarini nchini Qatar

Nukta ya mwisho ni kwamba hakuna yeyote kati ya mawaziri wakuu wawili hao, yaani anayeendesha serikali ya muda na aliyepewa jukumu la kuunda serikali mpya, aliye na nafasi nzuri ya kisiasa Lebanon. Hali hii ni mbaya zaidi kwa Hariri kwa sababu nchi anazozitegemea hazina ushawishi mkubwa ndani ya Lebanon. Kuhusu suala hilo, baadhi ya vyanzo vya habari vinasema kuwa Muhammad bin Salma, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia Arabia amesema kwamba Saudia haina imani tena na Saad Hariri kuwa waziri mkuu wa Lebanon na kwamba inafadhilisha nafasi hiyo ichukuliwe na Nawaf Salam.