Syria: Nchi za Magharibi uchaguzi wetu haukuhusuni ndewe wala sikio
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i70608-syria_nchi_za_magharibi_uchaguzi_wetu_haukuhusuni_ndewe_wala_sikio
Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amesema kuwa, nchi za Magharibi hazipaswi kujipa uthubutu wa kuzungumzia uchaguzi wa nchi hiyo kwani hauzihusu kwa mbali wala kwa karibu nchi hizo za kibeberu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 27, 2021 06:59 UTC
  • Syria: Nchi za Magharibi uchaguzi wetu haukuhusuni ndewe wala sikio

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amesema kuwa, nchi za Magharibi hazipaswi kujipa uthubutu wa kuzungumzia uchaguzi wa nchi hiyo kwani hauzihusu kwa mbali wala kwa karibu nchi hizo za kibeberu.

Faisal al Miqdad amenukuliwa na shirika la habari la SANA akisema hayo na kuongeza kuwa, wananchi wa Syria wamejitokeza kwa wingi ndani na nje ya nchi hiyo kutumia haki yao ya kuchaguzi viongozi wao na huo ni ujumbe maalumu kwa walimengu kuwa wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu ndio wenye haki ya kujiamulia mambo yao, si madola ajinabi.

Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Syria vile vile amesema, uchaguzi wa rais wa nchi hiyo umeonesha kuwa, wananchi wa Syria wako huru, wanatumia vizuri haki yao ya kidemokrasia na wanaonesha msimamo wao kupitia masanduku ya kura.

Aidha amesema, matamshi yaliyotolewa na baadhi ya nchi za Magharibi kuhusu uchaguzi wa Syria yanayonesha kuwa, nchi hizo haziishi katika dunia ya leo na ziko mbali sana na uhakika wa yanayoendelea sasa hivi ulimwenguni.

Rais Bashar al Assad wa Syria akishiriki katika uchaguzi wa rais siku chache zilizopita

 

Syria imealika waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi kutoka nchi rafiki kama vile Iran na Iraq kwa lengo la kushuhudia upigaji kura unavyofanyika. Kwa kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo, wananchi wa Syria kwa mara nyingine wametangaza uungaji mkono wao kamili kwa serikali yao suala ambalo linayachukiza mno madola ya kibeberu na vibaraka wao.

Juzi mawaziri wa mambo ya nje ya Ufaransa, Ujerumani, Italia, Uingereza na Marekani walidai kuwa uchaguzi huo hautakuwa huru wala haki.

Hii ni katika hali ambayo nchi hizo za Magharibi zikishirikiana na tawala vibaraka katika eneo zilituma magaidi wakufurishaji Syria mwaka 2011 ambao walianzisha vita kwa lengo la kuiangusha serikali halali ya Rais Assad.

Hata hivyo njama hiyo imesambaratika kutokana na oparesheni za jeshi la Syria kwa kushirikiana na harakati za muqawama na washauri wa kijeshi kutoka Iran na Russia.