Magaidi kadhaa wa Daesh watibiwa nchini Uturuki
Baadhi ya wanamgambo wa genge la kigaidi la Daesh hivi karibuni wamepatiwa matibabu kwa siri katika hospitali moja ya mji wa Gaziantep nchini Uturuki, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Syria.
Shirika la habari la Sputnik la nchini Russia limemnukuu daktari mmoja wa hospitali hiyo akiliambia shirika hilo katika mahojiano maalumu kwamba magaidi wanne wa Daesh walikuwa wamelazwa katika hospitali ya Ersin Arslan ya mkoa wa Gaziantep tarehe 5 Mei.
Magaidi hao wanaaminika ni kutoka kundi la Daesh ambao walijaribu kuingia nchini Syria karibu na eneo la Oguzeli, mkoani Gaziantep.
Daktari huyo amesema, wakati anawatibu magaidi nao waliwapata na majeraha ya risasi.
Ameliambia shirika la habari la Sputnik la nchini Russia kwamba: "Nadhani wakuu wa hii hospitali hawataki watu wajue kuwa watu hao wametibiwa hospitalini hapa."
Hata hivyo amesema, madaktari na wafanyakazi wa hospitali hiyo ya Ersin Arslan huwa wanagoma kuwatibu wanamgambo wa Daesh.
Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, Uturuki inatoa mafunzo kwa magenge ya kitakfiri yanayofanya mauaji nchini Syria na kuyarahisishia njia za kuingia Syria. Aidha serikali ya Uturuki inatuhumiwa kushirikiana na genge la Daesh kufanya biashara ya mafuta, ingawa serikali ya Ankara imekanusha madai hayo.