Ansarullah: Marekani inafadhilisha vita Yemen, haitaki amani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i71136-ansarullah_marekani_inafadhilisha_vita_yemen_haitaki_amani
Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen amelaani hatua ya Marekani ya kuliwekea vikwazo vipya taifa hilo la Kiarabu na kusisitiza kuwa, Washington inafadhilisha vita nchini Yemen, na wala haitaki amani kama inavyodai.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 11, 2021 03:25 UTC
  • Ansarullah: Marekani inafadhilisha vita Yemen, haitaki amani

Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen amelaani hatua ya Marekani ya kuliwekea vikwazo vipya taifa hilo la Kiarabu na kusisitiza kuwa, Washington inafadhilisha vita nchini Yemen, na wala haitaki amani kama inavyodai.

Mohammad Ali al-Houthi amesema hayo katika ujumbe alioutuma leo Ijumaa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kubainisha kuwa, tangazo la vikwazo vipya dhidi ya Wayemen lililotolewa jana na Wizara ya Hazina ya Marekani ni sehemu ya njama zilizoratibiwa kwa lengo la kuusambaratisha zaidi uchumi wa nchi hiyo maskini.

Ameeleza bayana kuwa, mielekeo hasi dhidi ya sekta binafsi ya Yemen, vikwazo dhidi ya Benki Kuu ya nchi hiyo, mashambulizi ya anga dhidi ya kampuni za uzalishaji na viwanda vya nchi hiyo, kuwahangaisha Wayemen kwa njaa kupitia mzingiro sambamba na kusimamisha mishahara kwa watumishi wa umma, yote hayo ni jinai na njama zilizopangwa makhsusi kwa ajili ya kuvuruga uchumi dhaifu wa nchi hiyo.

Ali al-Houthi ameongeza kuwa, "Marekani inafadhilisha chaguo la vita dhidi ya Yemen, na wakati huohuo inajidai kuwa muungaji mkono wa amani. Kutangaza vikwazo kwa kisingizio cha kutafuta amani ni kizingiti cha kupatikana amani yenyewe."

Masaibu ya watoto wa Yemen

Hivi karibuni pia, Mwenyekiti huyo wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen alisema hatua ya Marekani ya kutangaza eti imeliondoa jina la Ansarullah katika orodha yake ya makundi ya kigaidi ni hadaa tupu na mchezo mchafu wa kisiasa; kwani nchi hiyo maskini ya Kiarabu ingali chini ya vikwazo, mzingiro, ugaidi na uvamizi.

Hadi sasa Wayemeni zaidi ya elfu 16 wameshauawa katika vita vya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia kwa uungaji mkono wa hali na mali na nchi za Magharibi zikiongozwa na US, tokea Machi 2015, huku makumi ya maelfu ya wengine wakijeruhiwa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.