Taliban yapongeza kuondoka askari wa Marekani Bagram
Kundi la Taliban limesema Afghanistan imepiga hatua moja mbele kuelekea katika amani na uthabiti, wakati huu ambapo Marekani inawaondoa wanajeshi wake wote nchini humo.
Msemaji wa Taliban, Zabihullah Mujahid amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa, kundi hilo linapongeza na kukaribisha kwa mikono miwili hatua ya Marekani kuwaondoa askari wake wote katika kambi ya kijeshi ya Bagram.
Mujahid amebainisha kuwa, karibuni hivi, Waafghani watapata uthabiti na amani kamili baada ya vikosi vyote ajinabi kuondoka nchini humo. Kuondoka kwa wanajeshi hao katika kambi ya Bagram kunaashiria kumalizika vita vya Marekani dhidi ya Afghanistan vilivyodumu kwa karibu miaka 20.
Msemaji wa Taliban alisema hayo jana Ijumaa, masaa machache baada ya Washington kutangaza kuwa, askari wote wa Marekani na wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO wamekwishaondoka katika kambi ya Bagram. Kabla ya hapo, Zabihullah Mujahid alinukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kuwa, kuondoka vikosi ajinabi nchini humo kumewafungulia mlango wananchi wa Afghanistan wa kuamua wenyewe mustakabali wanaoutaka.
Sherehe za Kabul kukabidhiwa kambi ya kijeshi ya Bagram ambayo pia imekuwa ikitumika kama seli ya kuwazuilia maelfu ya raia wa Afghanistan, zinatazamiwa kufanyika leo Jumamosi.
Hii ni katika hali ambayo, duru za habari zimearifu kuwa, huenda wanajeshi elfu moja wa Marekani wakabaki nchini Afghanistan eti kwa ajili ya kulinda ubalozi wa US mjini Kabul na Uwanja wa Ndege mjini hapo.