Kukosolewa hatua ya Imarati ya kuwapatia uraia Wazayuni
Ikiwa ni katika mwendelezo wake wa kuimarisha uhusiano wake na utawala haramu wa Israel, serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) imechukua hatua ya kuwapatia uraia Wazayuni.
Nchi ya Kiarabu ya Imarati ilianza kutekeleza hatua za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Israel Septemba mwaka jana (2020).
Katika kipindi cha miezi kumi iliyopita utawala wa Imarati umechukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuimarisha uhusiano wake na utawala bandia wa Israel, ambapo kufunguliwa ubalozi wa Imarati mjini Tel-Aviv, kufunguliwa ubalozi wa Israel mjini Abu Dhabi na safari ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Israel huko Abu Dhabi ni miongoni mwa hatua muhimu katika uwanja huo.
Wakati huo huo, moja ya hatua nyingine iliyofanywa ni safari ya raia wa Kizayuni huko Imarati na wenzao wa Imarati huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Duru mbalimbali zimeripoti kwamba, katika kipindi cha miezi michache iliyopita, Imarati imewapatia uraia wa nchi hiyo takribani Wazayuni 5,000.
Mtandao wa Emirates Leaks ambao ni mashuhuri kwa kufichua habari za ndani na za nyuma ya pazia nchini Imarati umetangaza katika ripoti yake ya hivi karibuni ukiinukuu duru moja ya kuaminika lakini bila kuitaja jina ya kwamba, takribani raia 5,000 kutoka Palestina inayokaliwa kwa mabavu wamepatiwa uraia wa Imarati katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Hatua hiyo inafanyika katika kivuli cha uwekezaji nchini Imarati hususan katika miji miwili muhimu ya Dubai na Abu Dhabi. Maafisa wa serikali ya Imarati wanawaruhusu wawekezaji na wafanyabiashara kuchukua uraia wa nchi hiyo pasi na kuacha uraia wao wa asili. Kimsingi Imarati inadai kwamba, kwa kutoa uraia huo inafanya juhudi za kuwavutia wawekezaji wa kigeni, na hili ndilo jambo lililoisukuma nchi hiyo ya Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel.
Hatua hiyo ya Imarati iimechangamkiwa mno na raia kutoka Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel), hasa kwa kutilia maanani kwamba, wanapatiwa uraia wa Imarati na hawashurutishwi kuachana na uraia wao wa asili. Hatua hiyo ni fursa ya dhahabu kwani kwa kuwa na uraia wa Imarati Wazayuni hao sasa wanaweza kufanya safari kirahisi kabisa katika mataifa mengine ya Kiarabu bila kizingiti chochote.
Jarida la Kizayuni la Haaretz liliandika katika toleo lake la mwezi Februari mwaka huu kwamba: "Kupata uraia wa Imarati ni fursa kwa Wazayuni" kwa mujibu wa hati ya makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Abu Dhabi. Kupata uraia wa Imarati sio fursa kwa Wazayuni kwa ajili ya kupata kazi na ajira huko Abu Dhabi tu, bali Wazayuni hao watakuwa na uwezo wa kusafiri katika nchi ambazo awali ilikuwa ni marufuku kwao kufanya safari.
Hatua hiyo ya Imarati imekabiliwa na radiamali ya Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina. Tariq Salmi, msemaji wa Jihadul Islami ya Palestina amelaani hatua ya Imarati ya kuwapatia uraia wa nchi hiyo Wazayuni na kusema kuwa: Hatua hiyo ni doa jeusi kwa utawala saliti wa Imarati ambao umejidhalilisha kwa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel. Afisa huyo wa Jihadul Islami ameutaka utawala wa Imarati upige mahesabu yake upya hususan baada ya vya Seif al-Quds ambavyo vilithibitisha udhaifu wa adui Mzayuni na uimara wa muqawama katika kupigania haki za Wapalestina zilizoghusubiwa.
Nukta muhimu ni hii kwamba, upinzani dhidi ya hatua hii ya Imarati haujaishia kwa Wapalestina tu, bali hata ndani ya nchi hiyo hiyo ya Kiarabu kwenyewe ambapo raia na wanaharakati wa nchi hiyo wamekosoa vikali hatua hiyo wakibainisha kwamba, uamuzi huo unabadilisha muundo wa kijamii wa nchi hiyo.
Watumiaji wa mitandao ya kijami wameandika katika mitandoa hiyo kwamba, kumekuwa kukiendeshwa kwa siri zoezi la kuwapatia wageni kwa wigo mpana uraia wa nchi hiyo hususan Wazayuni; na hii ni katika hali ambayo, wakazi asili wa nchi hiyo ni wakimbizi, wako jela au wamepokonywa uraia.
Inaonekana kuwa, serikali ya Imarati inachukua hatua hizo na kutaka iwe kigezo cha kuigwa na mataifa mengine ya Kiarabu ya Ukanda wa Ghuba ya Uajemi kuhusiana na kadhia ya uhusiano na Israel. Hata hivyo wakosoaji wa hatua hiyo wanaamini kwamba, uamuzi huo wa Imarati utakuwa chimbuko la madhara makubwa ya kiutamaduni na kijami kwa nchi hiyo ya Kiarabu.