Najib Mikati apewa jukumu la kunda serikali nchini Lebanon
Najib Mikati mfanyabiashara tajiri wa Lebanon amepata wingi wa kura za Wabunge na hivyo kuidhinishwa kubeba jukumu la Uwaziri Mkuu na kuunda serikali ya nchi hiyo.
Najib Mikati aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Lebanon jana alipata kura 73 za Wabunge zinazomuuwezesha kuchukua rasmi jukumu la kuunda serikali ya baada ya aliyepewa jukumu hilo Saad al-Hariri kuachia ngazi hivi karibuni baada ya kupita miezi minane ya mkwamo wa kuunda serikali ya Lebanon.
Waziri Mkuu Hassan Diab ambaye serikali yake ilijiuzulu Agosti mwaka jana baada ya mlipuko wa Beirut ameendelea kuwa Waziri Mkuu wa serikali ya mshikizo hadi pale serikali mpya itakapoundwa.
Mara baada ya kupewa jukumu la kuunda serikali mpya ya Lebanon, Najib Mikati amesema: Ninahitajia imani ya wananchi hasa kwa kuzingatia kwamba, jukumu hili ni zito sana, lakini nitafanikiwa endapo pande zote zitatoa ushirikiano hitajika.
Mikati amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Lebanon mara mbili. Mara ya kwanza ni mwaka 2005 na baadaye kuanzia mwaka 2011 hadi 2014. Wananchi wa Lebanon hawana matumaini sana na Najib Mikati kama ataweza kuunda serikali katika kipindi hiki ambacho nchi hiyo imetawaliwa na hitilafu za mirengo ya kisiasa.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imetangaza kumuunga mkono Najib Mikati ambaye anakabiliwa na changamoto a kuunda serikali, na kubwa zaidi kuboresha hali ya kisiasa na kiuchumi endapo atafanikiwa kuvuka hatua ya kwanza ya kuunda serikali.