Taliban wasema wako tayari kushiriki kwenye serikali ya mpito ya Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i73442-taliban_wasema_wako_tayari_kushiriki_kwenye_serikali_ya_mpito_ya_afghanistan
Kundi la Taliban limetangaza kuwa liko tayari kushiriki katika serikali ya mpito ya Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 13, 2021 02:24 UTC
  • Taliban wasema wako tayari kushiriki kwenye serikali ya mpito ya Afghanistan

Kundi la Taliban limetangaza kuwa liko tayari kushiriki katika serikali ya mpito ya Afghanistan.

Kwa mujibu wa televisheni ya Al Jazeera, Suhail Shaheen, msemaji na mjumbe wa timu ya wawakilishi wa Taliban katika mazungumzo ya Doha, Qatar kati ya kundi hilo na serikali ya Afghanistan amesema, Taliban haijapokea pendekezo lolote jipya kutoka serika ya Kabul kuhusu mgawanyo wa madaraka, lakini iko tayari kushiriki katika serikali ya mpito ya nchi hiyo.

Shaheen amebainisha pia kuwa, kundi la Taliban halina nia ya kuiangusha serikali ya Afghanistan inayoongozwa na Rais Muhammad Ashraf Ghani.

Suhail Shaheen

Duru za habari katika mji mkuu wa Qatar, Doha zimetangaza kuwa, serikali ya Afghanistan imetangaza utayari wake wa kugawana madaraka na Taliban kwa sharti kwamba kundi hilo lisimamishe operesheni zake za kijeshi.

Tangu miezi takriban mitatu iliyopita, kufuatia tangazo la Marekani la kuondoa wanajeshi wake nchini Afghanistan, kundi la Talban limeshadidisha mashambulio na kuyateka maeneo mengi ya ardhi ya nchi hiyo.

Mapigano baina ya wanamgambo wa kundi hilo na vikosi vya serikali ya Kabul yangali yanaendelea katika pembe mbalimbali za Afghanistan.

Hii ni katika hali ambayo mazungumzo baina ya pande hizo mbili yanayolenga kuhitimisha vita na mapigano hadi sasa hayajazaa matunda.../