Kuanza duru mpya katika historia ya kisiasa ya Afghanistan
Baada ya wanamgambo wa Taliban kudhibiti mji mmoja baada ya mwingine na hatimaye kuudhibiti mji mkuu Kabul baada ya Rais Muhammad Ashraf Ghani kuikimbia nchi, sasa kumeanza duru mpya katika historia ya kisiasa ya nchi hiyo.
Baada ya miaka 20 (2001-2021) ya mapigano na askari wa kigeni na serikali ya Afghanistan, wanamgambo wa Taliban sasa wamo mbioni kuunda serikali nchini humo kwa mara ya pili katika kipindi cha miogo mitatu, huku kidhahiri wanamgambo hao wakiwa na mabadiliko ya namna fulani ikilinganishwa na miaka 20 iliyopita.
Taarifa iliyotolewa na kundi la wanamgambo wa Taliban baada ya kudhibiti mji mkuu Kabul na kurushwa hewani na Televisheni ya Taifa ya Afghanistan inaonyesha kuwa, kinyume na utawala wake wa hapo awali nchini humo, mara hii wanamgambo hao hawana nia ya kuzusha hofu, wasiwasi na wahaka miongoni mwa wananchi wa nchi hiyo. Katika taarifa hiyo imeelezwa bayana kwamba, watu wote ambao hapo kabla walikuwa wakifanya kazi na kushirikiana na wavamizi au hivi sasa wapo pamoja na serikali ya Kabul, wanamgambo wa Taliban wako tayari kuwapokea kwa mikono miwili kama ambavyo wametangaza msamaha kwa wote.
Taarifa yenye vipengee 13 ya kundi la wanamgambo wa Taliban pamoja na mambo mengine ina nukta ya kimsingi ambayo ni sisitizo la kudhamini usalama wa roho na mali za wananchi wote wa Afghanistan. Kimsingi nukta hii ndio inayoweza kuwa mstari wa kutenganisha baina ya Taliban ya huko nyuma na Taliban ya mara hii.
Katika mazingira ya hivi sasa swali ambalo limezishughulisha fikra na akili za wananchi, viongozi wa vyama, maafisa wa zamani wa serikali ya Afghanistan pamoja na walimwengu na mataifa mengine ya dunia ni hili kwamba, baada ya wanamgambo wa Taliban kuidhibiti Kabul na kuiangusha serikali ya Rais Muhammad Ashraf Ghani je wana mipango kwa ajili ya mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo?
Tukitupia jicho matamshi ya viongozi mbalimbali wa Taliban tutaona kuwa, sambamba na kukaribisha uundwaji wa serikali itakayojumuisha makundi, kaumu na shakhsia mbalimbali wa kisiasa wa nchi hiyo, yanatilia mkazo kwamba, serikali ijayo ya Afghanistan inapaswa kuwa ni ya Kiislamu lakini isiyo na fikra mgando.
Kupitia misimamo hiyo ya viongozi wa Taliban tunastafidi na nukta hii kwamba, kundi hilo linakusudia kufanyia marekebisho katiba ya Afghanistan na kuongezea baadhi ya vipengee kwa mtazamo na aidiolojia yao ambapo yumkini hilo likakinzana na asili ya utawala kuwa ni wa Jamhuri, wa kidemokrasia na unaozingatia uhuru wa mtu binafsi na wa kijamii ambayo haya kimsingi ni matakwa ya wananchi wa nchi hiyo.
Hasa kwa kutilia maanani kwamba, licha ya wanamgambo wa Taliban kuonekana kwamba, wamebadilisha baadhi ya mitazamo yao ikilinganishwa na miaka 20 iliyopita, lakini ni jambo lililo mbali wakalegeza kamba kuhusiana na kuunda utawala wa Kiislamu nchini humo.
Kwa kuzingatia moyo wa ‘mtaka yote’ ulioshuhudiwa kwa Taliban wakati wa kuanzishwa kundi hilo ni jambo lililo mbali likakabidhi mamlaka na uongozi kwa makundi na mirengo mingine baada ya kufanikiwa kurejea tena Kabul ikiwa ni baada ya kupita miaka 20 ya vita na umwagaji damu.
Kundi la wanamgambo wa Taliban linafahamu vyema kwamba, kama ilivyokuwa katika kipindi kifupi cha utawala wake hapo kabla nchini Afghanistan, haliwezi kufumbia macho nafasi ya kaumu na makundi mengine ya kisiasa na kimadhehebu katika kuunda serikali. Hata hivyo, kuna dhana hii kwamba, kundi hili linataka kuwa na hisa kubwa zaidi na halitakuwa tayari kugawana hisa sawa na mirengo mingine katika medani ya kisiasa ya Afghanistan.