Radiamali kwa hatua ya Iran ya kutuma mafuta Lebanon
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetuma meli za mafuta huko Lebanon kufuatia kupamba moto mgogoro wa nishati nchini humo.
Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah Alhamisi tarehe 19 mwezi huu wa Agosti alitoa hotuba kwa mnasaba wa Siku ya Ashura ya Imam Hussein (a.s) na kutangaza kuwa, meli zinazobeba mafuta kutoka Iran zimeelekea Lebanon. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukua hatua hiyo katika kipindi hiki ambapo Lebanon inakabiliwa na mgogoro wa nishati. Mgogoro huo umepelekea vituo vingi vya kuuzia petroli na dizeli, hospitali na hata maduka ya kuuzia mikate kufungwa huku wananchi wakiandamana kulalamikia hali hiyo.
Hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kutuma mafuta nchini Lebanon ambayo imechukuliwa kwa lengo la kuisaidia nchi hiyo kuondokana na mgogoro wa nishati, inaonyesha kuwa ndani ya Lebanon hakuna irada na azma ya kitaifa kwa ajili ya kuzipatia ufumbuzi changamoto za wananchi. Wakati huo huo baadhi ya shakshia na makundi ya kisiasa nchini humo yamedhihirisha namna yanayotanguliza mbele maslahi yao binafsi na ya kivyama kuliko maslahi ya wananchi na taifa.
Mara baada ya Katibu Mkuu wa Hizbullah kutangaza mpango huo wa kupeleka shehena ya mafuta huko Lebanon, baadhi ya wanasiasa, vyombo vya habari na televisheni zilizo dhidi ya Hizbullah hususan ndani ya Lebanon zilitangaza kuwa zina shaka kuhusiana na gharama za shehena hiyo ya mafuta kutoka Iran. Ni wazi kuwa, wale wanaopinga harakati ya muqawama wanaituhumu harakati ya Hizbullah ya Lebanon kuwa inaingilia masuala ya uchumi wa nchi hiyo na wamefanya kila wawezalo kuchafua taswira ya harakati hiyo. Pamoja na hayo, vyombo vya habari vya Lebanon vimetangaza kuwa, shehena hiyo ya mafauta kutoka Iran imenunuliwa na kundi ya wafanyabaishara wa Kishia wa Lebanon na si Hizbullah.
Saad Hariri pia amepinga waziwazi hatua ya kutumwa nishati na shehena ya mafuta ya Iran nchini Lebanon. Hariri ameandika jumbe 9 mtawalia akieleza upinzani wake dhidi ya hatua hiyo ya Iran na kusema, kuzipokea meli hizo za mafuta za Iran ni "njia ya kuelekea kuzimu". Hii ni licha ya kwamba, kiongozi huyo mwenye mielekeo ya Kimagharibi wa chama cha Machi 14 hakuwasilisha njia yoyote ya kutatua au hata kupunguza mgogoro wa nishati unaoisumbua Lebanon kwa sasa.
Ni wazi kuwa upinzani huo wa Hariri dhidi ya kupelekwa mafuta ya Iran nchini Lebanon hauna maslahi kwa taifa la nchi hiyo, bali zaidi ni msimamo uliochochewa na mivutano ya kisiasa ya ndani ya nchi. Hii ni kwa sababu, mwanasiasa huyo anadhani kwamba, hatua hiyo ya Iran itaboresha na kuimarisha nafasi ya Hizbullah na waungaji mkono wa kambi ya mapambano katika muundo wa utawala wa Lebanon. Katika upande mwingine msimamo huo wa Hariri unatokana na fikra za mrengo unaofanya mapatano na utawala haramu wa Israel katika eneo la Magharibi mwa Asia ambao una ajenda ya kudhoofisha kambi ya muqawama na mapambano.
Mkabala wa msimamo huu wa Saad Hariri na baadhi ya wanasiasa wa Lebanon, kuna msimamo wa Sayyid Hassan Nasrullah ambaye amezitahadharisha Marekani na Israel zisithubutu kushambulia meli hizo za mafuta kutoka Iran na kusisitiza kuwa, harakati hiyo ya mapambano inazitambua meli hizo kuwa ni sawa na ardhi ya Lebanon. Kwa maneno mengine ni kwamba, Katibu Mkuu wa Hizbullah anaweka mbele maslahi ya taifa la Lebanon kuliko maslahi yake binafsi na chama cha Hizbullah.
Utawala wa Kizayuni wa Israel pia umepinga hatua ya Iran ya kutuma shehena ya nishati nchini Lebanon. Japokuwa baraza la mawaziri la Israel halijatangaza rasmi upinzani wake dhidi ya suala hilo lakini waandishi na vyombo vya habari vya utawala huo wa Kizayuni vimeonesha hasira yao dhidi ya hatua hiyo ya Hizbullah na kuitaja kuwa ni pigo jingine dhidi ya Israel.
Inatupasa hapa kusisitiza kuwa, hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya kutuma shehena ya mafuta huko Lebanon imeonesha kuwa, Tehran inapiga jaribio lolote la kuibua machafuko na kuzidisha migogoro nchini humo. Vilevile inonesha kuwa, harakati ya Hizbullah haiwezi kuketi chini ya kusubiri hadi pale wanasiasa wanaowania madaraka, watakapoamua kuchukua hatua ya kupunguza matatizo yaliyopo.