UNIFIL yaikosoa Israel kwa kukiuka mamlaka ya kujitawala Lebanon
Hatua ya utawala haramu wa Israel ya kukiuka mamlaka ya kujitawala Lebanon wakati wa kuishambulia Syria imekosolewa na Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Mataifa huko Lebanon (UNIFIL)
Mapema Jumamosi 21 Agosti, kwa mara nyingine, ndege za utawala wa Kizayuni wa Israel zilikiuka anga ya Lebanon wakati wa kushambulia Syria. Kabla ya hapo pia utawala wa Israel umekuwa ukikiuka mara kwa mara mamlaka ya kujitawala Lebanon wakati wa kuishambulia Syria. Vitendo hivyo vya kichokozi vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Lebanon na Syria vinaweza kutathminiwa ifuatavyo.
Lebanon si nchi iliyo vitani kwa sasa na Israel. Vita vya mwisho vya Lebanon na Israel vilikuwa mwaka 2006 na baada ya kumalizika vita hivyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasishwa azimio nambari 1701 ambalo lilisisitiza ulazima wa kila upande kuheshimu mamlaka ya kijitawala ya upande wa pili. Katika hali ambayo Harakati ya Hizbullah ya Lebanon inafungamana na azimio hilo lakini utawala wa Kizayuni umelikiuka mara kadhaa.
Ukiukwaji huo umekaririwa sana katika miaka ya hivi karibuni wakati wa hujuma za mara kwa mara za utawala huo haramu dhidi ya Lebanon. Kutokana na uchokozi huo, Lebanon imekuwa ikilalamikia Baraza la Usalama ikitaka hatua za kivitendo zichukuliwe dhidi ya Israel. Hata hivyo, kutokana na ushawishi wa Marekani na kura yake ya turufu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halijaweza kuchukua hatua yoyote ya maana. Utawala wa Kizayuni wa Israel umepata kiburi cha kuendelea kukiuka anga ya Lebanon kutokana na kimya cha jamii ya kimataifa.
Ni kwa msingi huo ndio kufuatia kuendelea kukiukwa anga ya Lebanon mara kwa mara, Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Mataifa huko Lebanon (UNIFIL) kikatoa taarifa na kusema Israel imekiuka azimio la Umoja wa Mataifa. Kamanda wa UNIFIL, Meja Jenerali Stefano Del Col ametoa jibu kwa uchokozi wa Israel na kuandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa: "Kuruka ndege za kivita za Israel katika anga ya Lebanon ni ukiukwaji wa azimio 1701 na pia ni ukiukwaji wa mamlaka ya kujitawala Lebanon." Del Col ameongeza kuwa, " Kwa mara nyingine tunalitaka Jeshi la Israel lisitishe hatua zake hizo ambazo zinavuruga na kudhoofisha jitihada za UNIFIL za kupunguza taharuki na kujenga imani miongoni mwa wakaazi wa eneo."

Katika upande mwingine, vitendo hivyo vya uchokozi vya Israel vinalenga kuvuruga maslahi na usalama wa Syria. Ingawa utawala wa Kizayuni kwa miongo kadhaa sasa umekuwa ukikalia kwa mabvu Milima ya Golan ya Syria, lakini Syria haijaingia katika vita na utawala huo hasimu. Pamoja na hayo kwa miaka 10 sasa Syria imekuwa katika vita na magaidi kutoka mataifa mbali mbali na utawala wa Israel umetumia vita hivyo kama fursa ya kutoa pigo kwa Syria na hivyo kukiuka mamlaka ya nchi hiyo mara kadhaa kwa kutekeleza mashambulizi.
Israel imekuwa ikidai kuwa mahsambulizi yake Syria yanalenga kutoa pigo kwa ngome za harakati za mapamabano ya Kiislamu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi hiyo ya Kiarabu. Hata hivyo ni wazi kuwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Syria yana lengo la kuwaunga mkono magaidi walio katika nchi hiyo. Hivi sasa Jeshi la Syria, likiungwa mkono na waitifaki wake, limeweza kutoa pigo kubwa kwa magaidi. Israel ni kati ya pande ambazo hazitaki kuona mgogoro ukimalizika nchini Syria na zinaona kuendelea kuwepo mgogoro katika nchi hiyo kwa muda mrefu ni kwa maslahi yake. Kwa msingi huo utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukichukua hatua za kuwaunga mkono magaidi nchini Syria.
Kutokana na uhasama huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imewasilisha barua za malalamiko kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Katika barua hizo, Syria imesema mashambulizi mapya ya Israel ni katika fremu ya sera za jinai zenye lengo la kurefusha vita vya magaidi dhidi ya taifa la Syria. Aidha Syria imesema dunia inafahamu kuwa, lengo kuu la Israel katika uhasama wake ni kuyapa motisha makundi ya kigaidi na watenda jinai wengine kaskazini mashariki mwa ardhi ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na Marekani na pia eneo la kaskazini magharibi linalokaliwa kwa mabavu na Uturuki.