UNICEF: Ndani ya kila dakika 10, mtoto anaaga dunia Yemen
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) ametahadharisha kuhusu hali ya kibinadamu inayozidi kuwa mbaya nchini Yemen kutokana na vita vinavyoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu na kusema kuwa, mtoto mmoja wa Yemen hupoteza maisha kila baada ya dakika 10.
Henrietta Fore alisema hayo jana Jumatatu alikihutubu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na hali ya kibinadamu nchini Yemen na kueleza kuwa, "Nchini Yemen, mtoto mmoja anafariki dunia ndani ya kila dakika 10 kutokana na sababu zinazozuilika kama vile utapiamlo na magonjwa yanayoweza kudhibitiwa kupitia chanjo."
Amebainisha kuwa, "Miaka 6 iliyopita, watu wazima walianzisha vita Yemen. Walichukua hatua hiyo licha ya kufahamu matokeo mabaya ya migogoro ya namna hii kwa watoto wadogo."
Afisa huyo wa ngazi ya juu wa UNICEF amekumbusha kuwa, watoto milioni 11.3 wa Yemen wanahitajia misaada ya kibinadamu, huku milioni 2.3 miongoni mwao wakisumbuliwa na utapiamlo wa kiwango cha juu.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, lishe duni miongoni mwa watoto wa Yemen walio chini ya umri wa miaka mitano ni ya kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika historia.
Aidha hivi karibuni Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) ulionya kuwa, mustakabli wa elimu ya watoto zaidi ya milioni 6 nchini Yemen upo hatarini kwani watoto hao wamo katika hatari ya kukosa masomo kutokana na kushindwa kwenda shuleni.