Kuundwa serikali ya Taliban nchini Afghanistan
Serikali ya mpito iliyoundwa na wanamgambo wa Taliban nchini Afghanistan imeanza rasmi kazi zake.
Zabiullah Mujahid, msemaji wa kundi la wanamgambo wa Taliban amesema kuwa, serikali hiyo ya muda haijaundwa kwa mujibu wa hisa na mgawo wa kikaumu, hata hivyo kundi hilo linafanya juhudi ili kuhakikisha kwamba, kaumu na matabaka yote ya jamii ya Afghanistan yanakuwa na nafasi na mchango serikalini.
Kwa mujibu wa orodha iliyotangazwa na Taliban, Mullah Muhammad Hassan Akhund ameteuliwa kuwa Waziri Mkuu na kiongozi wa serikali hiyo huku Mullah Abdul-Ghani Baradar akipewa wadhifa wa Naibu Waziri Mkuu.
Tukitupia jicho orodha na safu ya uongozi iliyotangazwa tunaona kuwa, akthari ya wajumbe wa serikali hiyo ni maafisa na viongozi waandamizi wa kundi la Taliban. Matamshi ya msemaji wa Taliban kwamba, serikali hiyo haijaundwa kwa kuzingatia hisa na mgawo wa kikaumu nchini Afghanistan inaunga mkono nadharia hii kwamba, kundi hilo halijazingatia suala la hisa na mgawo wa kikaumu na matabaka ya nchi hiyo.
Licha ya matamshi ya mara kwa mara na sisitizo la viongozi waandamizi wa Taliban baada ya kuchukua hatamu za uongozi kwamba, wataunda serikali jumuishi, lakini orodha ya mawaziri iliyotangazwa hivi sasa inaonyesha kuwa, Taliban imekiuka ahadi yake ya hapo awali ya kuunda serikali shiriki na itakayojumuisha makundi na matabaka yote. Licha ya sisitizo la huko nyuma la wasemaji wa kundi la Taliban la kuunda serikali jumuishi nchini Afghanistan na kuandaa mazingira na anga mwafaka kwa ajili ya ushiriki wa kaumu na matabaka yote katika mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo, lakini haikuwa ikitabiriwa kwamba, kundi hilo litafanya mambo hivyo na kutoa fursa kulingana na uwezo wa mirengo na jamii ya nchi hiyo.
Kwa kuzingatia kuwa kwa mujibu ya Katiba ya Afghanistan mawaziri wanaopendekezwa kwa ajili ya kuongoza wizara mbalimbali wanapaswa kupigiwa kura na Bunge, hadi sasa bado haifahamika kama Taliban itafuata mkondo huo wa kisheria au mawaziri hao wataanza kutekeleza majukumu yao pasi na kusubiri kupigiwa kura ya kuwa na imani nao katika Bunge la Afghanistan.
Hatua ya kundi la wanamgambo wa Taliban ya kutangaza orodha ya baraza lake la mawaziri inaonyesha kuwa, wanamgambo hao hawana nia kabisa ya kuzishirikisha kaumu na mirengo mingine ya kisiasa katika serikali. Hivyo basi hata madai ya kufanyika mashauriano na pande zingine katika kuunda serikali hiyo, ni jambo ambalo kwa hakika haliwezi kukubaliwa na fikra za waliowengi.
Katika hali ambayo sambamba na wanamgambo mwa Taliban kutangaza orodha yao ya mawaziri hawakuashiria hata kwa mbali juu ya kuwasilisha orodha hiyo Bungeni ili ipigiwe kura, tunaweza kusema kuwa, kwa uoni wa kundi hilo ni kwamba, asasi hiyo haina nafasi yoyote kwa serikali ya Taliban na hakuna mpango wa kuheshimu hilo kwa mujibu wa Katiba ya Afghanistan. Endapo kundi la Taliban halitawasilisha orodha yake ya baraza la mawaziri Bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura, basi kitendawili cha kundi hilo cha kuundwa mfumo wa Imarati ya Kiislamu kitakuwa kimeteguliwa.
Kwa kuzingatia kwamba, katika siku za hivi karibuni kumekuwa kukisikika miito mbalimbali kutoka kwa wajumbe wa Baraza la Uongozi la Taliban la kufanyiwa marekebisho Katiba ya Afghanistan na kulitaja hilo kama takwa la makundi ya kisiasa ya nchi hiyo, kuna uwezekano pia wa katiba hiyo kufanyiwa marekebisho kwa maslahi ya mfumo wa Imarati ya Kiislamu.
Kwa kuzingatia kuwa, Mullah Muhammah Akhund yupo katika uongozi mpya wa kisiasa na angali pia ni kiongozi wa kundi la Taliban inaonekana kuwa, mfumo wa Imarati ya Kiislamu ambayo unaongozwa na Amir umo katika hali ya kukamilika uundaji wake.
Inaonekana kuwa, wanamgambo wa Taliban wakiwa na nia ya kuzuia malalamiko na upinzani zaidi katika mazingira ya sasa wamekuwa hawatamki wazi juu ya kufanya hima ya kuunda Imarati ya Kiislamu, lakini kivitendo kila kitu kinaonekana wazi kwamba, watafanya juhudi za kuunda mfumo huo hatua kwa hatua.