Sep 12, 2021 07:44 UTC
  • Wabahrain waandamana wakipinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel

Wananchi wa Bahrain wameendelea kupinga hatua ya nchi yao ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel unaotenda jinai kila uchao dhidi ya wananchi wa Palestina.

Jana usiku wananchi wa Bahrain waliandamana na kupaza sauti wakipinga mwenendo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel unaoikalia kwa mabavu Palestina.

Waandamanaji hao mbali na kutoa nara za kulaani kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala unaotenda mauaji wa Israel wameutaka utawala wa kifamilia wa Manama kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa na kusisitiza kwamba, wafungwa hao wa kisiasa wanapaswa kuachiliwa huru bila masharti.

Bahrain imekuwa ikilalamikiwa na asasi mbalimbali za kieneo na kimataifa za kutetea haki za binadamu kwa kuendesha ukandamiizaji dhidi ya raia hususan wapinzani wa utawala wa al-Khalifa.

Maandamano ya kupinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel

 

Hivi karibuuni Marta Hurtado, msemaji wa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu alisisitiza katika mkutano na waandishi wa habari kuwa, kamishna wa haki za binadamu Michelle Bachelet anasikitishwa sana na utumiaji nguvu na ukatili unaofanywa na askari usalama na polisi wa Bahrain kwa ajili ya kuzima mgomo katika jela ya nchi hiyo. 

Tangu Februari 14, 2011 hadi sasa, Bahrain imekuwa uwanja wa mapambano ya amani ya wananchi dhidi ya utawala wa kiimla wa Aal Khalifa; na tangu wakati hadi sasa raia zaidi ya 11,000 wametiwa nguvuni kwa tuhuma bandia na idadi kubwa ya wapinzani wa utawala huo wa kifamilia wamevuliwa uraia.

Tags