Jeshi la Iraq lakanusha: Muda wa kuwepo kijeshi Marekani haujarefushwa
(last modified 2021-11-20T12:21:45+00:00 )
Nov 20, 2021 12:21 UTC
  • Jeshi la Iraq lakanusha: Muda wa kuwepo kijeshi Marekani haujarefushwa

Msemaji wa kamandi ya operesheni za pamoja za Iraq amesema muda wa kuwepo wanajeshi wa Marekani nchini humo haujarefushwa.

Tahseen al-Khaffaji amebainisha kuwa, kauli za uvumi zinazotolewa kuhusu kurefushwa muhula wa kuondoka vikosi vya jeshi la Marekani si sahihi na akasisitiza kwamba. tarehe ya kuondoka askari wa vitani wa Marekani inajulikana kuwa ni Desemba 31 na hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanywa.

Al Khaffaji ameongeza kuwa, uhusiano kati ya nchi mbili baada ya kuondoka vikosi vya askari wa vitani utakuwa wa kiwango cha mashauriano katika masuala ya utoaji mafunzo, silaha, intelijensia na usalama dhidi ya kundi la kigaidi la DAESH (ISIS).

Tarehe 26 Julai mwaka huu, Baghdad na Washington zilikubaliana kuwa, askari wa vitani wa Marekani wataondoka nchini Iraq ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, lakini askari wengine wachache, ambao idadi yao haijajulikana, watasalia nchini humo kwa ajili ya kutoa ushauri na mafunzo kwa askari wa jeshi la Iraq.

Magaidi wa kundi la ukufurishaji la DAESH (ISIS)

Wakati huohuo, kamati ya uratibu na mashauriano ya makundi ya muqawama ya Iraq, imetoa taarifa kuhusiana na kuondoka askari wa Marekani katika ardhi ya nchi hiyo na kusisitiza: "Tunafuatilia kwa karibu kuona vifungu vya kile kilichotajwa kuwa ni mazungumzo ya kistratejia vinaheshimiwa kwa kiwango gani na tunawafuatilia kwa uzito mkubwa wavamizi na ahadi walizotoa, ukiwa ni upande mmoja wa makubaliano ambao hatuna imani nao."

Ijapokuwa zimeshafanyika duru kadhaa za mazungumzo ya kistratejia kati ya Baghdad na Washington kwa ajili ya kuhitimisha kuwepo kijeshi Marekani nchini Iraq kutokana na kukamilika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la DAESH (ISIS), sambamba na kupitishwa na bunge la Iraq pia mpango wa kuondolewa wanajeshi wote wa kigeni nchini humo, lakini Marekani ingali inakiuka mpango huo na kuendelea kubaki katika ardhi ya nchi hiyo.../

 

Tags