110 wauawa, kujeruhiwa katika mripuko wa bomu Msikitini Pakistan
Waislamu wasiopungua 45 wameuawa shahidi leo wakati wa Swala ya Ijumaa katika shambulizi la kigaidi lililofanyika ndani ya msikiti mmoja ulioko katika mji wa Peshawar nchini Pakistan.
Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa, mripuko wa bomu umetikisa msikiti huo ulioko katika eneo la Kocha Risaldar, ambapo mbali na watu zaidi ya 45 kuuawa, wengine zaidi ya 65 wamejeruhiwa.
Ijaz Ahsan, afisa wa ngazi ya juu wa polisi katika kituo kikuu cha polisi cha Peshawar amethibitisha kutokea mripuko huo wa bomu na kufafanua kuwa, maiti 45 zimeonekana mpaka sasa ndani ya msikiti huo.
Ahsan ameeleza kuwa, watu wasiopungua 65 wamejeruhiwa kwenye tukio hilo, na wamepelekwa katika Hospitali ya Lady Reading mjini hapo kwa ajili ya matibabu.
Afisa huyo wa polisi amesema washambuliaji wawili waliwapiga risasi walinzi nje ya msikiti huo, na dakika chache baada ya kuingia ndani ya eneo hilo la ibada, sauti kubwa ya mripuko ikasikika.

Afisa mwingine wa polisi mjini Peshawar, Waheed Khan ameliambia shirika la habari la AP kuwa, magaidi hao waliingia katika msikiti huo wakati ambao ummati mkubwa wa Waislamu walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya Swala ya Ijumaa.
Hadi tunamaliza kuandaa habari hii, hakuna kundi lililokuwa limetangaza kuhusika na hujuma hiyo inayosadikika kuwa ya kigaidi.