Hizbullah yatangaza mshikamano na wananchi mashujaa wa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i82588-hizbullah_yatangaza_mshikamano_na_wananchi_mashujaa_wa_palestina
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetangaza mshikamano wake na wananchi wa Palestina na kuyatolea wito mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kutekeleza majukumu yao katika kuitetea Quds Tukufu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 17, 2022 02:21 UTC
  • Hizbullah yatangaza mshikamano na wananchi mashujaa wa Palestina

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetangaza mshikamano wake na wananchi wa Palestina na kuyatolea wito mataifa ya Kiarabu na Kiislamu kutekeleza majukumu yao katika kuitetea Quds Tukufu.

Maghasibu wa Kizayuni juzi Ijumaa kwa mara nyingine tena waliushambulia na kuhujumu Msikiti Mtukufu wa al Aqsa ambacho ni kibla cha kwanza cha Waislamu na kuibua mapigano kati yao na Wapalestina. Wapalestina zaidi ya 150 walijeruhiwa na wengine 400 walitiwa nguvuni na wanajeshi wa Israel. Wapalestina 17 wameuliwa shahidi tangu siku 15 zilizopita hadi kufikia jana Jumamosi. 

Televisheni ya al Manar imeripoti kuwa, harakati ya Hizbullah imetoa taarifa ikilaani mashambulizi ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu katika Msikiti wa al Aqsa; mashambulizi ya kinyama dhidi ya waumini wa Palestina waliokwenda hapo kwa ajili ya Swala, hujuma dhidi ya wakazi wa mji wa Quds na kuharibiwa mali zao. 

Mashambulizi ya Wazayuni dhidi ya Wapalestina huko al Aqsa 

Hizbullah imesisitiza kuwa iko pamoja na wananchi wa Palestina ambao wanaendelea kupambana na kuutetea Msikiti wa al Aqsa huko Quds; na wakati huo huo imepongeza ujasiri na mapambano ya kishujaa ya raia hao wa Palestina dhidi ya wanajeshi makatili wa Israel. 

Harakati hiyo ya muqawama ya Lebanon aidha imesema: Kile kilichofanywa juzi na wanajeshi ghasibu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ni ukiukaji mkubwa na kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa. Hizbullah imezitaka jumuiya za OIC, Arab League, nchi na mataifa ya Waislamu duniani kutekeleza majukumu yao ya kidini na kisheria mkabala wa vitendo vya kigaidi vya utawala wa Kizayuni ili kuwasaidia Wapalestina kadiri inavyowezekana.