Al Kadhimi: Wapiganaji wa Daesh hawana chaguo isipokuwa kifo
(last modified Sat, 23 Apr 2022 11:29:56 GMT )
Apr 23, 2022 11:29 UTC
  • Al Kadhimi: Wapiganaji wa Daesh hawana chaguo isipokuwa kifo

Waziri Mkuu wa Iraq amewambia magaidi wa Daesh (ISIS) kwamba wanasubiriwa na mashambulizi zaidi na mauaji ya kiongoi mpya wa kundi hilo.

Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al-Kadhimi amesema wakati wa kukagua awamu ya pili ya Operesheni Azma Imaral huko magharibi mwa mkoa wa al Anbar kwamba Jeshi la Iraq linapata ushindi baada ya mwingine huku magaidi wa Daesh wakiendelea kupata vipigo na kushindwa. 

Al-Kadhimi ameongeza kuwa: "Viongozi wa kundi la Daesh wanaangamizwa mmoja baada ya mwingine na hawana chaguo isipokuwa kifo."

Al-Kadhimi pia ameviambia vikosi vya wapiganaji wa kujitolea vya al Hashdul Shaabi kwamba: “Nyinyi ndio mnaolinda heshima ya nchi na ardhi yake, mnaandika historia na kung'oa mizizi ya ugaidi Iraq na duniani.” 

Katika siku za hivi karibuni, baada ya kusambazwa faili la sauti inayohusishwa na msemaji wa Daesh akitishia kufanya mashambulio ya kigaidi ili kulipiza kisasi mauaji ya kiongozi wa kundi hilo, Abdullah Qardash na msemaji wake Abu Hamza al-Qurashi, Waziri Mkuu wa Iraq alitoa taarifa akivitaka vikosi vya usalama kuongeza kiwango cha utayarifu katika miji mbalimbali ya nchi.

Licha ya kushindwa kundi la Daesh nchini Iraq mnamo Novemba 2017, lakini wapiganaji wa kundi hilo la kigaidi bado wanafanya mashambulio ya kushtukiza katika baadhi ya maeneo ya Iraq.