Mripuko wa bomu lililotegwa ardhini waua watu 26 kaskazini mashariki mwa Nigeria
Watu wapatao 26 wameuawa na wengine watatu wamejeruhiwa wakati magari mawili yalipokanyaga bomu la kutegwa ardhini katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria, ambacho ni kitovu cha waasi.
Shirika la Kimataifa la Usalama, ambalo hutoa huduma za usalama kwa mashirika ya kigeni yasiyo ya kiserikali kaskazini mashariki mwa Nigeria limetangaza kuwa, magari mawili yaliyokuwa yakitembea kati ya miji ya Rann na Gamboru Ngala yalikanyaga bomu la kutegwa ardhini IED.
Taarifa ya shirika hilo imesema, mripuko huo umesababisha "vifo vya watu 26 na kujeruhi watatu". Hata hivyo Polisi ya jimbo la Borno haikuweza kutoa maoni yake mara moja kuhusiana na tukio hilo lililotokea hapo jana.
Wapiganaji wa Boko Haram na makundi mengine ya waasi katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi wamekuwa wakipambana na vikosi vya usalama kwa zaidi ya miaka 15 kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na mara nyingi hutumia mada za miripuko kuwalenga raia na vikosi vya usalama.
Liman Tom, raia msafiri katika barabara lilipojiri tukio hilo amesema magari hayo mawili yameharibika vibaya na manusura walikimbizwa hospitalini na askari wa kikosi kazi cha pamoja cha wananchi waliofika kwenye eneo la tukio.../