Ansarullah yawapongeza Wapalestina kwa kusimama kidete kuulinda Msikiti wa al Aqsa
(last modified Mon, 30 May 2022 10:19:19 GMT )
May 30, 2022 10:19 UTC
  • Ansarullah yawapongeza Wapalestina kwa kusimama kidete kuulinda Msikiti wa al Aqsa

Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen imelipongeza taifa la Palestina kwa kusimama kiume kukihami na kukilinda Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa katika siku ya "Maandamano ya Bendera."

Mapema jana Jumapili, walowezi wa Kizayuni walianza kuuvamia Msikiti wa al Aqsa kwa ajili ya kufanya sherehe zinazoitwa "Maandamano ya Bendera." Huku wakiwa wamepewa ulinzi kamili wa wanajeshi makatili wa Israel, zaidi ya walowezi 1,000 wa Kizanyuni walivamia eneo la Msikiti wa al Aqsa na kufanya vitendo mbalimbali vya kihalifu vya kuwachochea Waislamu.

Ilipofika jioni hiyo jana, maelfu ya walowezi wa Kizayuni walivamia sehemu inayoitwa Bab al 'Amud katika eneo la kale la mji wa Quds wakafanya sherehe hizo kwa jeuri na uadui mkubwa huku wakitoa maneno ya kejeli na istihzai kwa Waislamu na matukufu yao.

Nembo ya Ansarullah ya Yemen

 

Tovuti ya Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen imetoa taarifa na kutangaza kuwa, vitendo vya kichochezi vya adui na walowezi wa Kizayuni katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds, na jinai yao ya kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa kwa ulinzi kamili wa wanajeshi wa Israel ambao wamewaweka nguvuni makumi ya Wapalestina, yote hayo yanamlazimisha kila mwenye fikra huru alaani jinai hiyo bila ya kujali rangi, kabla wala taifa lake.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, sherehe za "Maandamano ya Bendera" zimefanyika katika hali ambayo, makundi ya muqawama ya Palestina yaliuonya mara chungu nzima utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba ndio utakaobeba dhima na lawama za lolote litakalotokea iwapo utafanya sherehe hizo ambazo Israel huwa inasherehekea siku ilipoanza kulikalia kwa mabavu eneo la mashariki la mji mtakatifu wa Quds.