Jun 18, 2022 11:28 UTC
  • Iraq yatakiwa kuchunguza wizi wa mafuta yanayopelekwa Israel

Serikali ya Iraq imetakiwa ifanye uchunguzi wa kina kuhusu wizi wa mafuta ya nchi hiyo katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Kurdistan, kaskazini mwa nchi na kupelekwa katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.

Mwanasiasa wa kujitegemea katika eneo la Kurdistan, Othman Hassan Pasha ameliambia shirika la habari la al-Maalomah kuwa, "Si siri tena wizi wa mafuta kutoka Kurdistan kwenda Tel Aviv unafanyika chini ya uangalizi wa vyama vinavyotawala Erbil."

Amesema kuna meli tatu zinazofanya magendo hayo katika bandari ya Uturuki, na mchakato mzima huo unaungwa mkono kikamilifu na serikali ya Ankara.

Mwanasiasa huyo wa Kurdistan amefichua kuwa, mapipa kati ya 40,000 hadi 80,000 ya mafuta ghafi yanawasili katika bandari za utawala haramu wa Israel kila wiki kwenye magendo hayo. 

Amesema magendo hayo ya mafuta yamewaathiri mamilioni ya wakazi wa eneo la Kurdistan, huku bidhaa muhimu zikiendelea kupanda madukani.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Iran, Russia na Uturuki hivi karibuni zilitoa taarifa zikilaani wizi wa mafuta unaofanywa na Marekani nchini Syria. 

Tags