Walowezi wa Kizayuni wafanya maandamano Quds, wavamia al-Aqsa
Maelfu ya walowezi wa Kizayuni wamefanya maandamano ya kutiliwa shaka mashariki mwa Quds inayokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel na kuzusha hali ya taharuki katika eneo hilo.
Maandamano hayo ya jana Jumapili yamefanyika wakati huu ambapo Wapalestina na Waislamu wote kwa ujumla wanaingia katika mwezi mtukufu wa Ramadhani. Aidha maandamano hayo tata yamesadifiana na maadhimisho ya miaka 49 ya kukaliwa kwa mabavu Quds Tukufu na utawala haramu wa Israel.
Vurumai zilizuka katika maandamano hayo, wakati walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya kufurutu ada walipotishia kuteketeza moto Masjidul Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu na kukabiliana na Wapalestina katika eneo hilo. Imearifiwa kuwa, Wazayuni 208 walivamia Msikiti huo Mtakatifu wakiwa chini ya ulinzi na himaya ya maafisa wa polisi wa utawala katili wa Israel. Hata hivyo walinzi wa Msikiti huo waliwazuia baadhi ya walowezi hao kutekeleza baadhi ya matambiko yao katika eneo hilo tukufu.
Hadi sasa zaidi ya Wapalestina 210 wameshauawa shahidi na utawala haramu na wa Kizayuni wa Israel tangu lilipozuka wimbi la Intifadha ya Quds Oktoba mwaka jana, huku wengine wengi wakiendelea kuitiwa mbaroni.