Safari ya kwanza ya Bashar Assad mjini Aleppo (Halab)
(last modified Sun, 10 Jul 2022 07:10:04 GMT )
Jul 10, 2022 07:10 UTC
  • Safari ya kwanza ya Bashar Assad mjini Aleppo (Halab)

Rais Bashar al-Assad wa Syria aliutembele mji wa Aleppo (Halab) siku ya Ijumaa na sambamba na kushiriki katika swala ya Eid al-Adha, alizindua miradi kadhaa ya kiuchumi na maendeleo katika mji huo.

Uzinduzi wa miradi na safari katika mji huo ni jambo linaloonyesha wazi kwamba Assad ana nia na azma madhubuti ya kuurejesha mji huo katika nafasi yake ya zamani na anafanya kazi kwa bidii kuelekea lengo hilo. Kabla ya Aleppo kukabiliwa na mradi wa uasi ulioanza kutekelezwa na maadui mwaka 2011, ulichukuliwa kuwa mji mkuu wa kiuchumi wa Syria, na Asad mweneyewe pia alifanya juhudi kubwa za kuboresha hali ya kiuchumi na kibiashara ya mji huo mara tu baada ya kuingia madarakani mwaka 2000.

Mji wa Aleppo ulinawiri sana kiuchumi kabla ya maadui kuanza kutekeleza mradi wa kuiangusha serikali halali ya Bashar al-Asad na hilo lilitokana na mapatano mazuri ya kiuchumi na ujirani mwema yaliyokuwa yakitekelezwa kabla ya mradi huo. Lakini kwa bahati mbaya kufuatia mradi huo wa wapinzani na maadui wa Syria, ambapo, kwa masikitiko makubwa, Uturuki pia ilishiriki kwa muda, si tu mchakato wa kuboresha na kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi mbili ulisimama, bali vita vilivyodumu kwa miaka kadhaa viliuharibu kabisa mji wa Aleppo vikiwemo vituo vyake muhimu vya kiuchumi na kitamaduni.

Rais Bashar al-Asad (katikati) akikagua miradi ya maendeleo mjini Aleppo

Hata hivyo baada ya kukombolewa mji huo mwaka 2016, serikali ya Syria ilianza mara moja juhudi za kuurejesha mji huo katika nafasi yake ya awali, na katika uwanja huo, miradi ya ujenzi mpya na ukarabati iliwekwa kwenye ajenda ya serikali. Kwa kuzingatia hilo, miradi miwili mikubwa ya umeme na maji imezinduliwa katika safari ya karibuni ya Asad katika mji huo, miradi ambayo bila shaka itakuwa na nafasi muhimu katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo katika mji huo.

Bila shaka, jambo muhimu zaidi linaloweza kuleta utulivu, kuharakisha na kudhamini mchakato wa kuikarabati Syria, hususan mji wa Aleppo na kuufanya kuwa tena kitovu muhimu cha kiuchumi na kibiashara cha Syria, ni kudumishwa utulivu na usalama na kuzuiwa migogoro yoyote nchini humo na hasa katika mpaka wake na Uturuki. Ni wazi kuwa hilo linaweza tu kutimia iwapo mikataba ya zamani ya usalama na amani kati ya nchi hizo itahuishwa na kuheshimiwa. Hii ni kwa sababu mikataba hiyo inadhamini usalama wa mipaka ya Uturuki na mamlaka ya kujitawala taifa la Syria.

Kwa kuzingatia kwamba miradi ya uharibifu na mapinduzi dhidi ya serikali ya Damascus, na hasa katika eneo la kaskazini mwa Syria inatekelezwa kutoka nje ya mipaka ya nchi hiyo ni wazi kuwa tatizo hilo linaweza kutatuliwa tu kwa njia ya mazungumzo kwa ajili ya kudhamini usalama wa Uturuki na kuheshimiwa utawala wa kitaifa wa Syria pamoja na kulindwa ardhi zake zote. Tunaweza kusema bila kusita kwamba, katika kipindi ambacho uhusiano na ushirikiano wa mataifa mawili hayo ulikuwa katika kilele chake mwishoni mwa muongo wa 2000 ni watu wa mataifa hayo ndio walionufaika zaidi na hali hiyo na bila shaka ni nchi mbili hizo ndizo zilidhurika zaidi baada ya uhusiano huo kuharibika kufuatia matukio ya mwaka 2011 na kuendelea.

Hivi sasa pia ambapo serikali ya Syria imeupa tena kipaumbele ukarabati wa Aleppo, ni wazi kuwa Uturuki ambayo ina ukaribu wa kijiografia na Syria, ndiyo itakayonufaika zaidi na hali hiyo ikiwa itaamua kuimarisha uhusiano wake na serikali ya Damascus la sivyo itaendelea kuziletea nchi hizo na eneo zima kwa ujumla hasara na madhara yasiyofidika.

Askari wa Syria baada ya kuukomboa mji wa Aleppo

Hata kama baadhi ya vyombo vya habari vimetathmini ziara ya Bashar Asad mjini Aleppo kuwa ina ujumbe wa onyo kwa Uturuki kuhusu matokeo ya utekelezaji operesheni mpya ya uchochezi, lakini kwa uchache katika mazingira ya sasa, hakuna ushahidi wowote unaoashiria uwepo wa operesheni kama hiyo, na kwa hiyo ni wazi kuwa ziara ya Bashar al-Asad mjini Aleppo imezingatia zaidi maendeleo na ukarabati wa mji huo kuliko jambo jingine lolote, ambapo Uturuki inaweza kufaidika kwa kuboresha uhusiano wake na Syria na kutumia uzoefu wa miaka ya huko nyuma kwa ajili ya kupunguza gharama za kuingilia masuala ya ndani ya Syria.