Bahrain inaongoza kwa idadi ya wafungwa wa kisiasa Uarabuni
Kituo cha Haki za Binadamu cha Bahrain (BCHR) kimesema Bahrain inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wafungwa wa kisiasa miongoni mwa nchi zote za Kiarabu.
Taarifa ya asasi hiyo ya kutetea haki za binadamu Bahrain imesema vyombo vya usalama vya utawala wa Manama vinawashikilia wafungwa wa kisiasa zaidi ya 4,500 katika jela mbalimbali za nchi hiyo.
Kituo cha Haki za Binadamu cha Bahrain kimeeleza kuwa, mamlaka za Bahrain zimewatia mbaroni watu zaidi ya 15,000 kutokana na misimamo yao ya kisiasa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
Asasi za kutetea haki za binadamu zimetahadharisha kuhusiana na ukandamizaji mkubwa unaofanywa nchini Bahrain na vyombo vya usalama dhidi ya raia na kutaka kukomesha vitendo hivyo.
Mara kwa mara, wananchi wa Bahrain wamekuwa wakiandamana kuwaunga mkono wafungwa wa kisiasa wa nchi hiyo na kutoa wito wa kuachiliwa huru wafungwa hao wanaoshikiliwa katika magereza ya utawala wa kifalme wa Aal Khalifa.
Utawala huo wa kiimla umekuwa ukikandamiza wapinzani tangu ulipotumia mkono wa chuma mwaka 2011 kwa msaada wa utawala wa Saudi Arabia kupambana na maandamano ya umma ya kupigania mageuzi ya kidemokrasia.
Mbali na adhabu za vifungo, utawala wa Aal Khalifa umewafutia uraia pia mamia ya Wabahrain katika kesi bandia zilizoendeshwa kwa umati na mahakama za utawala huo.