Mrithi wa Ufalme Bahrain apewa mwaliko na Netanyahu
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa zamani wa Israel anayetazamiwa kuunda serikali mpya ya utawala wa Kizayuni amemualika Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Bahrain, Salman bin Hamad Aal Khalifah kuitembelea ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kupachikwa jina la Israel.
Gazeti la The Times of Israel limeripoti kuwa, Netanyahu jana Jumapili alizungumza kwa njia ya simu na Bin Hamad Aal Khalifa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Bahrain, na kumualika kuitembelea Israel eti kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa pande mbili.
Gazeti hilo la Kizayuni limeeleza kuwa, Netanyahu amemueleza Mrithi wa Ufalme wa Bahrain kwamba, pande mbili hizo zina 'fursa kubwa' za eti kuimarisha uhusiano wao.
Utawala wa kiukoo wa Aal-Khalifa unachukua hatua za kuimarisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel, licha ya pingamizi na lalama za wananchi wa Bahrain.
Ikumbukwe kuwa mwaka 2020 utawala wa kifalme wa Bahrain ulisaini na utawala haramu wa Israel makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia baina ya pande mbili kwa upatanishi wa rais wa Marekani wakati huo Donald Trump.
Hata hivyo tangu wakati huo hadi sasa, upinzani wa wananchi wa Bahrain kwa hatua hiyo ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu umekuwa kizuizi kikubwa kwa ustawishaji wa uhusiano kati ya Manama na Tel Aviv.