Nov 22, 2022 07:17 UTC
  • Yemen yazima jaribio la meli ajinabi kuiba mafuta yake

Vikosi vya jeshi la Yemen vimetangaza habari ya kufanikiwa kuzima jaribio la wizi wa mafuta ya nchi hiyo, lililofanywa na meli ya kubeba mafuta ya nchi ya kigeni.

Brigedia Jenerali Yahya Saree, Msemaji wa Jeshi la Yemen amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kueleza kuwa: Vikosi vya Yemen vimefanikiwa kuitimua meli ya mafuta iliyojaribu kuelekea katika bandari ya al-Dhaba, kusini mwa nchi.

Amesema vikosi hivyo vilimazimika kufanya operesheni ya kuilazimisha meli hiyo kuondoka haraka, baada ya mabaharia wa meli hiyo ya kigeni kupuuza maonyo ya vikosi hivyo vya usalama vya Yemen.

Brigedia Jenerali Saree amebainisha kuwa, meli hiyo ya mafuta ya nchi ajinabi ilikuwa inapanga kuiba kiwango kikubwa cha mafuta ya Wayemen kusini mwa nchi.

Ameongeza kuwa: Vikosi vya ulinzi na usalama vya Yemen vitaendelea kulinda mamlaka ya kujitawala na rasimali za nchi hiyo, ili mapato yake yawasaidie Wayemen na yalipe mishara ya wafanyakazi katika maeneo yote ya Yemen.

Bandari ya Hudaydah ya Yemen

Hivi karibuni, Waziri wa Ulinzi wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen aliashiria njama za muungano wa vita wa Saudi Arabia za kupora utajiri wa Yemen na kusisitiza kuwa, operesheni ya uporaji wa mali za Yemen haitapita bila jibu.

Julai mwaka huu, meli ya mafuta ya Imarati ilipakua mapipa 400,000 ya mafuta yasiyosafishwa yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 43.6 kutoka bandari ya Razum katika jimbo la Shabwah.

Kabla ya hapo, zaidi ya mapipa milioni mbili ya mafuta ghafi yenye thamani ya takriban zaidi ya dola milioni 270 yaliporwa kutoka bandari ya Al-Shahr katika mkoa wa Hadramaut nchini Yemen.

Tags