Je, India itasalimu amri mbele ya mashinikizo ya Trump?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i129266-je_india_itasalimu_amri_mbele_ya_mashinikizo_ya_trump
Siku ya Jumatano, Agosti 6, Rais Donald Trump wa Marekani alitia saini amri ya kuweka ushuru wa ziada wa asilimia 25 dhidi ya bidhaa za India ili kukabiliana na hatua ya nchi hiyo ya kuendelea kununua mafuta ya Russia, na hivyo kuongeza ushuru jumla kwa bidhaa za India hadi asilimia 50.
(last modified 2025-08-08T02:11:50+00:00 )
Aug 08, 2025 02:11 UTC
  • Je, India itasalimu amri mbele ya mashinikizo ya Trump?

Siku ya Jumatano, Agosti 6, Rais Donald Trump wa Marekani alitia saini amri ya kuweka ushuru wa ziada wa asilimia 25 dhidi ya bidhaa za India ili kukabiliana na hatua ya nchi hiyo ya kuendelea kununua mafuta ya Russia, na hivyo kuongeza ushuru jumla kwa bidhaa za India hadi asilimia 50.

Trump, ambaye hadi sasa ameshindwa kutimiza ahadi yake ya kampeni ya kusitisha mara moja vita kati ya Ukraine na Russia, anaiadhibu India kwa kununua mafuta kutoka nchi hiyo ili kuishinikiza Moscow. Ameishutumu India kwa kununua "kiasi kikubwa cha mafuta ya Russia" na kisha kuyauza kwenye soko la wazi kwa faida kubwa. Ameitaja tabia hii kuwa ni kutozingatia vita vya Ukraine na kutishia kuongeza ushuru huo hadi asilimia 100.

Licha ya shinikizo jipya la ushuru la Marekani kwa India, kuna ushahidi unaoonyesha kwamba New Delhi haitasalimu mbele ya mashinikizo hayo ya Washington. Narendra Modi Waziri Mkuu wa India amesisitiza kuendelea kuagiza mafuta kutoka Russia na kuwataka raia wanunue bidhaa zinazozalishwa nchini kwao. Vyanzo vya serikali ya India pia vinasema kuwa mikataba ya muda mrefu ya mafuta na Russia haiwezi kufutwa kwa urahisi na kwamba uagizaji wa bidhaa utaendelea.

Wizara ya Mambo ya Nje ya India pia imekosoa vikali ushuru huu na kuutaja kuwa sio wa haki. Wizara hiyo imelaani vikali ushuru wa ziada wa asilimia 25 uliowekwa na Trump dhidi ya mauzo ya nje ya India kwenda Marekani, kwa kisingizio cha ununuzi wa New Delhi mafuta ya Russia, na kusisitiza kuwa itachukua hatua zote zinazohitajika kwa ajili ya kulinda maslahi ya kitaifa ya India.  imesema katika taarifa: "Tayari tumeweka wazi msimamo wetu kuhusu suala hili; uagizaji wetu unatokana na mazingira ya soko na unalenga kuhakikisha usalama wa nishati kwa watu bilioni 1.4 wa India." Taarifa hiyo pia imesema uamuzi wa Washington wa kutoza ushuru wa ziada wa asilimia 25 kwa bidhaa za India zinazouzwa Marekani "ni wa kusikitisha sana," na kuongeza: "Tunasisitiza kwamba hatua hizi si za haki, hazihalalishiki na hazina mantiki."

India, nchi ya tatu kwa uagizaji mafuta ghafi duniani baada ya China na Marekani, kihistoria imekuwa ikinunua mafuta yake mengi kutoka Asia Magharibi, lakini hali hii ilibadilika baada ya Russia kulazimika kuuza mafuta yake kwa bei ya chini kutokana na vikwazo vya nchi za Magharibi, na hivyo kuifanya India kuwa mnunuzi mkubwa wa mafuta ya Russia sambamba na Uchina.

Donald Trump na Narendra Modi wa India

Ushuru mpya wa Donald Trump kwa India, ambao sasa unafikia asilimia 50, ni jibu la moja kwa moja kwa New Delhi kutokana na kuendelea kununua mafuta ya Russia. Hatua hiyo ina madhara makubwa ya kisiasa na kiuchumi. Athari za kiuchumi ni pamoja na kuongezeka kwa gharama ya kusafirisha bidhaa za India kwenda Marekani, hasa katika sekta kama vile nguo, dawa na teknolojia ya habari, kupungua ushindani wa bidhaa za India katika soko la Marekani na uwezekano wa kudorora uchumi wa India iwapo mivutano ya kibiashara itaendelea.

Ama kuhusu taathira za kijiografia za ushuru huo wa Marekani kwa India,  tunaweza kutaja kuongezeka kwa mvutano kati ya Washington na New Delhi, ambayo inaweza kuathiri usalama na ushirikiano wa kimkakati kati ya pande hizo, na hivyo kuongeza uwezekano wa kuwekewa vikwazo washirika wengine wa kibiashara wa Russia kama vile Uchina na Brazil.

Wakati huo huo, ushuru mpya wa Trump dhidi ya India, unaweza kuwa na taathira kubwa za muda mrefu kwa uhusiano wa India na Marekani. Katika hatua ya kwanza, tunapasa kuashiria mvutano wa kidiplomasia kati ya Marekani na India na kupungua uaminifu wa kimkakati kati ya pande mbili. Ushuru wa asilimia 25 hadi 50 kwa bidhaa za India, hasa katika sekta kama vile nguo, dawa, vito na vipuri vya magari, unaonyesha kupungua imani ya Washington kwa New Delhi. Suala jingine ni kwamba India imekataa kufuata kibubusa msimamo wa Marekani kuhusu vita vya Ukraine, na hali hii ya India kutoegemea upande wowote imemkasirisha Trump. New Delhi inasisitiza kwamba hatua zake katika nyanja za kigeni, kama vile kununua mafuta kutoka Russia, zinatokana na maslahi ya kitaifa ya India, na kwamba Washington haina haki ya kuamrisha au kuiburuza India katika uwanja huo.

Pili, tunapasa kuashiria kudhoofika ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili. Mauzo ya India kwa Marekani yalikuwa ya dola bilioni 87 mwaka uliopita ambapo ushuru wa sasa unaweza kusababisha hasara ya hadi dola bilioni 7 kila mwaka. Kampuni ndogo na za kati za India ziko hatarini zaidi kufuatia ushuru huo mpya wa Trump, hasa wa asilimia 50, ambapo zinaweza kukabiliwa na kupungua kwa mapato na upotezaji ajira.

Tatu, tishio la vita vya ushuru kati ya Marekani na India kwa usalama na ushirikiano wa kikanda linapaswa kuzingatiwa. Mivutano ya kibiashara inaweza kuathiri ushirikiano wa usalama wa India na Marekani katika eneo la India na Pasifiki, hasa katika kukabiliana na ushawishi wa China katika mfumo wa Mkataba wa Pande Nne za Marekani, India, Australia na Japan. Pia, mikataba ya kibiashara baina ya nchi mbili, ambayo ilipaswa kuongeza biashara hadi dola bilioni 500 ifikapo 2030, sasa inakabiliwa na hatari kubwa.

Suala la mwisho kuzingatia ni jibu la India kwa mashinikizo makubwa ya Marekani, ambayo yalikuwa hayajawahi kushuhudiwa tena huko nyuma. Jibu hili limechukua sura ya mapambano na kukaa ngangari. India hadi sasa imepinga mashinikizo ya Marekani ya kufungua soko lake la ndani, na kuchukulia kutetea maisha ya wakulima wake kuwa mstari mwekundu kwa nchi hiyo. Wakati huo huo serikali ya Modi pia imejaribu kutuliza hali ya mambo kwa kupunguza ushuru kwa baadhi ya bidhaa za Marekani, lakini mafanikio yake yamekuwa madogo. Kwa ujumla, ushuru huu unaweza kuhamisha mahusiano ya India na Marekani kutoka njia ya ushirikiano wa kimkakati hadi ushindani na kutoaminiana.