Wataalamu: Netanyahu 'hana ubavu' wa kukabiliana na wanamapambano wa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i94378-wataalamu_netanyahu_'hana_ubavu'_wa_kukabiliana_na_wanamapambano_wa_palestina
Wataalamu mbalimbali wa kijeshi wa Israel wametoa maneno makali ya kumlaumu waziri mkuu mwenye misimamo ya kufurutu ada, Benjamin Netanyahu na kusema kuwa, hana uwezo wa kukabiliana na mashambulio ya makombora ya wanamapambano wa Palestina.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 23, 2023 10:08 UTC
  • Wataalamu: Netanyahu 'hana ubavu' wa kukabiliana na wanamapambano wa Palestina

Wataalamu mbalimbali wa kijeshi wa Israel wametoa maneno makali ya kumlaumu waziri mkuu mwenye misimamo ya kufurutu ada, Benjamin Netanyahu na kusema kuwa, hana uwezo wa kukabiliana na mashambulio ya makombora ya wanamapambano wa Palestina.

Mtandao wa Kizayuni wa Walla umeripoti habari hiyo na kuwanukuu wataalamu mbalimbali wa kijeshi wa Israel wakiviambia vyombo vya habari vya utawala huo kwamba makundi ya muqawama ya Palestina yamekuja na mlingano mpya katika medani ya vita, na kwamba Benjamin Netanyahu hana uwezo wa kukabiliana nao.

Wamesema, hivi sasa tukio lolote lisilo la kawaida linalofanywa na Wazayuni katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linajibiwa kwa mvua ya makombora kutoka Ghaza yanayopiga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Mtaalamu  mwingine Mzayuni amesema, serikali ya Netanyahu sasa imeamua kunyamazia kimya mashambulio ya mara kwa mara ya makombora ya Wapalestina na hata majibu yanayotolewa na Israel yanazidi kuwa dhaifu.

Makomandoo wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS

 

Wakati huo huo msemaji wa jeshi la utawala wa Kizayuni amesema kuwa, ving'ora vya tahadhari vimepigwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vya Sderot na Ashkelon baada ya kuanza mashambulizi ya makombora ya wanamapambano wa Palestina wa Ukanda wa Ghaza.

Leo Alkhamisi pia, kumeripotiwa taarifa za mashambulizi ya anga ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika baadhi ya maeneo ya Ukanda wa Ghaza.

Majibu ya wanamapambano wa Palestina yamekuja baada ya wanajeshi makatili wa Israel kuvamia mji wa Nablus wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kwa ajili ya kuwatia mbaroni baadhi ya Wapalestina. Wapalestina 11 waliuwa shahidi na 102 walijeruhiwa katika uvamizi huo wa jana Jumatano wa wanajeshi dhalimu wa Israel huko Nablus.