Arab League, Hizbullah zakaribisha kuhuishwa uhusiano wa Iran, Saudia
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) imekaribisha makubaliano ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia wa Iran na Saudi Arabia, miaka saba baada ya kuvunjika uhusiano huo.
Katibu Mkuu wa Arab League, Ahmed Aboul Gheit amesema kufikiwa mapatano hayo kwa upatanishi wa China, kutatamatisha hali ya taharuki iliyokuwepo baina ya Iran na Saudi Arabia kwa kipindi cha miaka saba.
Mwanadiplomasia huyo wa Misri amesema muafaka huo utafungua ukurasa mpya si tu kwenye mahusiano ya nchi mbili hizo, lakini pia miongoni mwa nchi za Asia Magharibi, sambamba na kuimarisha uthabiti katika eneo.
Wakati huohuo, Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuhuishwa uhusiano wa kidiplomasia wa Iran na Saudi Arabia ni pigo kubwa kwa 'mradi' wa Marekani na Israel katika eneo la Mashariki ya Kati.
Sheikh Naim Qassem amesma hayo katika ujumbe wa Twitter na kueleza bayana kuwa, makubaliano hayo baina ya Tehran na Riyadh kwa upatanishi wa Beijing yanaashiria mwanzo wa mambo mazuri kwa mataifa ya eneo hili la kistratajia.
Huku hayo yakiarifiwa, Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Berri amezipongeza Iran na Saudia kwa kufikia mapatano ya kuhuisha uhusiano wao wa kidiplomasia na kuongeza kuwa, irada ya kukurubiana ina nguvu kuliko ile ya kutengana na kufarikiana.
Aidha makundi mbalimbali ya muqawama wa Wapalestina yamekaribisha makubaliano hayo na kusisitiza kuwa, yanatumai mapatano hayo yataunga mkono haki ya watu wa Palestina ya kupambana kwa ajili ya kurejesha haki zao za kihistoriana na kuwa na matokeo chanya kwa kadhia ya Palestina.
Katika mazungumzo yaliyofanyika Ijumaa ya juzi kati ya Iran na Saudi Arabia mjini Beijing kwa upatanisha wa China, nchi hizo mbili zilikubaliana kurejesha uhusiano wa kidiplomasia baada ya kukatwa kwa miaka saba.