GCC: Mapatano ya Saudia, Iran kuhitimisha migogoro katika eneo
Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (GCC) limepongeza makubaliano ya hivi karibuni kati ya Iran na Saudi Arabia ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia uliokuwa umevunjika kwa kipindi cha miaka saba.
Taarifa ya Baraza la Mawaziri la umoja huo wa Waarabu iliyotolewa mwishoni mwa kikao chake cha 155 imesema kuwa, mapatano hayo ni hatua chanya katika kupatiwa ufumbuzi mivutano na kuhitimisha migogoro katika eneo la Asia Magharibi.
Taarifa hiyo imesema makubaliano baina ya Iran na Saudia kwa upatanishi wa China yamefungua ukurasa mpya katika kuimarika uhusiano wa kiuchumi na kiusalama baina ya Tehran na Riyadh.
Mawaziri wa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (GCC) wamesema katika taarifa hiyo kuwa, wanatumai mapatano hayo yataimarisha uhusiano miongoni mwa mataifa ya eneo katika misingi ya maelewano, kuheshimiana, ujirani mwema, sanjari na kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine pamoja na kufungamana na Hati ya Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).

Siku chache zilizopita pia, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) walipongeza makubaliano hayo kati ya Iran na Saudi Arabia ya kuhuisha uhusiano wao.
OIC ilisema mapatano hayo yataimarisha usalama na utulivu wa Ghuba ya Uajemi na katika nchi za Kiarabu kwa ujumla sambamba na kuimarisha umoja wa Kiislamu.
Baada ya siku kadhaa za mazungumzo mazito yaliyoandaliwa na China, Iran na Saudi Arabia hatimaye zilifikia makubaliano Ijumaa ya Machi 10, ambapo ziliafikiana kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na kufungua tena balozi ndani ya miezi miwili.