Maafisa wa Iran, Lebanon wazungumzia matukio ya kieneo mjini Beirut
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i95462-maafisa_wa_iran_lebanon_wazungumzia_matukio_ya_kieneo_mjini_beirut
Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Mahusiano ya Kigeni la Iran, Kamal Kharrazi amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah mjini Beirut, ambapo wamejadili matukio ya hivi sasa ya kisiasa na kiusalama katika eneo la Asia Magharibi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 24, 2023 04:21 UTC
  • Maafisa wa Iran, Lebanon wazungumzia matukio ya kieneo mjini Beirut

Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Mahusiano ya Kigeni la Iran, Kamal Kharrazi amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah mjini Beirut, ambapo wamejadili matukio ya hivi sasa ya kisiasa na kiusalama katika eneo la Asia Magharibi.

Kharrazi amesisitiza kuwa, uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya nchi nyingine na miamala ya kibabe ya Marekani na utawala haramu wa Israel kuhusiana na Wapalestina ni mambo muhimu ambayo yamechangia mno kukosekana amani na uthabiti katika eneo hili.

Afisa huyo ambaye ni waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu imewanyooshea mkono wa urafiki majirani zake wote na anatumai kwamba nchi za eneo hili zitashirikiana katika kuimarisha usalama na utulivu wa eneo hili zima.

Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mojtaba Amani, Balozi wa Iran mjini Beirut wameshiriki pia katika mazungumzo hayo baina ya Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Mahusiano ya Kigeni la Iran na Sayyid Nasrullah.

Kharrazi (kushoto) na Rais Assad wa Syria

Mbali na kukutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana pia na kuzungumza na maafisa wengine wa ngazi ya juu wa Lebanon, akiwemo Spika wa Bunge la nchi hiyo ya Kiarabu, Nabih Berri.

Kabla ya kuelekea Lebanon, Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Mahusiano ya Kigeni la Iran aliitembelea Syria na kukutana na viongozi wa nchi hiyo ya Kiarabu, akiwemo Rais Bashar al-Assad.