HAMAS: Mapambano dhidi ya Israel yataendelea mpaka Aqsa ikombolewe
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema mapambano yao kwa kushirikiana na makundi mengine ya muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel yataendelea hadi pale Msikiti wa al-Aqsa utakapokombolewa.
Ali al-Amoudi, Mkuu wa Idara ya Habari ya HAMAS katika Ukanda wa Gaza alisema hayo jana Ijumaa akihutubia umati mkubwa wa waandamanaji wa Kipalestina wanaounga mkono muqawama, mji mtukufu wa Quds na eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu.
Al-Amoudi ameeleza kuwa, ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Palestina unaofanywa na Wazayuni maghasibu unachochea vita vya kidini katika maeneo matukufu ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu mjini Quds.
Amesisitiza kuwa, "Makundi yote ya (muqawama) ya Palestina yameungana katika mapambano dhidi ya utawala haramu wa Israel, huku Gaza kikiwa kichwa cha mkuki wa mapambano hayo."
Kabla ya hapo, Salah al-Aruri, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS alibainisha kwamba, wanamuqawama katu hawatauruhusu utawala ghasibu wa Israel uendelee kuuvunjia heshima msikiti huo mtakatifu hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Siku chache zilizopita, makumi ya walowezi wa Kizayuni wenye misimamo mikali waliuvamia tena Msikiti wa al-Aqsa chini ya ulinzi mkali kutoka kwa wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel.
Walowezi hao wa Kizayuni wakisaidiwa na kupewa himaya na jeshi la Israel baada ya kuingia katika eneo la ndani la msikiti huo mtakatifu walisikika wakipiga nara dhidi ya Uislamu na Waislamu na kufanya vitendo vya kuchochea hisia za Waislamu.
Vitendo vya hujuma za walowezi wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa al-Aqsa vimekithiri zaidi baada ya kuingia madarakani serikali yenye misimamo mikali ya Benjamin Netanyahu ambayo imekuwa ikionyesha chuki za wazi wazi dhidi ya Wapalestina na maeneo yao matakatifu.