Kushadidi hatua zisizo za kiutu za Israel dhidi ya Wapalestina
Utawala wa Kizayuni wa Israel umeanza kuchukua hatua kali zisizo za kiutu dhidi ya Wapalestina ili kufikia malengo yake ya kujipanua.
Kuhusiana na suala hilo, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu, ametoa amri ya kuwekwa sheria kali za ujenzi kwa ajili ya Wapalestina.
Netanyahu aidha amesema litatolewa fungu maalumu la fedha kusaidia upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Kwa mujibu wa ripoti ya mpango huo, Meya wa utawala wa Kizayuni katika mji wa Baitul Muqaddas ana mpango wa kuanzisha mradi wa ujenzi wa kitongoji kipya katika ardhi za uwanja wa ndege wa zamani katika eneo la Ut'airut lililoko baina ya miji miwili ya Ramallah na Baitul Muqaddas.
Wakati huohuo, utawala wa Kizayuni ambao nia yake ni kubadilisha muundo wa demografia na idadi ya watu kwa maslahi ya Wazayuni unabomoa nyumba za Wapalestina kwa visingizio hewa kama vya kutokuwa na vibali vya ujenzi.
Katika hatua ya kutaka kuidhibiti na kuizima Intifadha ya Quds, utawala wa Kizayuni wa Israel umeweka adhabu kali ikiwemo kubomoa nyumba za Wapalestina wanaoshriki kwenye Intifadha hiyo na kuzitoa familia za watu hao katika nyumba zao.
Kitambo nyuma Umoja wa Mataifa ulibainisha wasiwasi ulionao kutokana na ubomoaji wa nyumba za Wapalestina tangu kuanza mwaka huu wa 2016 na kutangaza kuwa idadi ya nyumba zilizobomolewa katika miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu ni nyingi zaidi kuliko nyumba zote za Wapalestina hao zilizobomolewa katika mwaka uliopita wa 2015.
Katika upande mwengine utawala wa Kizayuni umekuwa ukiwakatia maji mara kwa mara Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi hususan katika msimu huu wa joto na wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Hatua hiyo ya kinyama imezidisha matatizo ya Wapalestina na hata kuwafanya baadhi yao walazimike kuhama. Na hii ni katika hali ambayo tangu mwaka 1967 hadi sasa, utawala haramu wa Israel umewaachia Wapalestina watumie asilimia 15 tu ya haki yao ya mgao wa maji na kupora asilimia 85 nzima ya maji hayo.
Wakati huohuo ofisi ya kitaifa ya kulinda ardhi na ya muqawama dhidi ya ujenzi wa vitongoji imetahadharisha kuhusu matokeo hatari ya wito wa viongozi wa kidini wa Kizayuni wenye misimamo ya kufurutu mpaka kwa walowezi wa Kizayuni kwa madhumuni ya kutoa mashinikizo kwa Wapalestina. Ofisi hiyo imeeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina katika vijiji na maeneo yao.
Sholumu Malmid, mkuu wa baraza linalojiita 'baraza la marabbi wa vitongoji vya Kizayuni' amewataka walowezi wa Kizayuni wayatie sumu maji ya kunywa ya vijiji na maeneo ya Wapalestina katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan, wawaibie mali zao na kuharibu mashamba yao ya zaituni.
Hii ni pamoja na kwamba askari wa utawala wa Kizayuni kila uchao wanavamia maeneo na nyumba za Wapalestina na kuwaua shahidi, kuwajeruhi au kuwatia nguvuni wananchi hao madhulumu. Tangu Oktoba 2015, yaani wakati ilipoanza Intifadha ya Quds hadi sasa, zaidi ya Wapalestija 215 wameshauliwa shahidi na maelfu ya wengine wamejeruhiwa au kutiwa nguvuni.
Utawala khabithi wa Kizayuni unashadidisha jinai zake hizo kwa lengo la kuwapigisha magoti Wapalestina ili wasalimu amri na kughairi kuendeleza muqawama wao dhidi ya Uzayuni.
Ikumbukwe kuwa moja ya masharti aliyotoa Avigdor Lieberman, waziri mpya wa vita wa Kizayuni la kukubali kushika wadhifa huo ni kuendelezwa sera za "mauaji ya kigaidi dhidi ya Wapalestina".
Historia ya miaka 68 ya kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu Palestina inaonyesha kuwa ugaidi ulioratibiwa unaotekelezwa kwa sura tofauti na utawala wa Kizayuni umekuwa siku zote katika ajenda zinazofanyiwa kazi na waasisi na viongozi wa utawala huo wa haramu.../