Viongozi 6 hatari wa Daesh watiwa nguvuni Iraq
Idara ya Intelijinsia ya Iraq imetangaza kuwatia mbaroni watu sita wanaotajwa kuwa magaidi hatari sana wa kundi la Daesh (ISIS) katika mkoa wa Nineveh nchini humo.
Mwaka 2017 Iraq ilitangaza kupata ushindi na kutoa kipigo kwa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) baada ya kundi hilo kudhibiti theluthi moja ya ardhi ya Iraq kwa muda wa miaka mitatu na nusu. Hata hivyo licha ya ushindi huo wa Iraq, masalia na vibaraka wa kundi la Daesh wapo katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo wakiendelea kufanya hujuma za kigaidi.
Idara ya Intelijinsia ya Iraq imearifu kuwa, vingozi sita hatari wa kundi la Daesh ambao wamekamatwa katika mkoa wa Nineveh kaskazini mwa nchi hiyo wamehusika katika makabiliano na vyombo vya usalama na kuwashambulia raia.
Magaidi hao wa Daesh walikuwa na mahusiano na makundi ya kijeshi ya "General Camps Brigade, Yarmouk , Eiser Asri, Zat al Sawari na Dabiq". Magaidi hao waliotiwa nguvuni walikuwa wakipewa pesa kwa hatua yao ya kuwa na mfungamano na makundi hayo ya kigaidi.