Wamarekani weusi, wahanga wa kwanza wa ubaguzi katika ajira
Takwimu za hivi karibuni nchini Marekani zinaonyesha kuwa, watu weusi wanaunda asilimia 90 ya wafanyakazi walioachishwa kazi mwaka huu kutokana na kuongezeka kwa hofu ya mdororo wa kiuchumi na sera ya makampuni mengi ya kupunguza wafanyakazi.
Gazeti la Washington Post limeandika kuwa: Kwa mujibu wa data kutoka Ofisi ya Takwimu za Kazi, Wamarekani weusi wanaunda karibu asilimia 90 ya watu wazima ambao wamepoteza kazi tangu mwezi Aprili mwaka huu. Vilevile kulingana na data zilizotolewa hivi karibuni ya Wakala wa Shirikisho, wafanyikazi 267,000 kati ya 300,000 waliopoteza kazi katika miezi ya hivi karibuni walikuwa Wamarekani weusi.
Sera ya ubaguzi ndio sera ya msingi katika sekta mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi za Magharibi; na kutokana na ongezeko la mivutano ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, watu wasio wazungu, wafuasi wa dini na jamii za waliowachache kama Waislamu na wanawake wako chini ya mashinikizo zaidi kuliko matabaka mengine.
Takwimu zilizochapishwa za kufukuzwa kazi watu weusi katika jamii ya Marekani mwaka huu zinaonyesha kuwa, kuna pengo kubwa katika kiwango cha ukosefu wa ajira baina ya Wamarekani weusi na weupe, kiasi kwamba wimbi la kufukuzwa wafanyikazi katika tasnia ya teknolojia na huduma mwaka huu limewalenga watu weusi. Ripoti zinazonyesha kuwa, tayari makampuni makubwa ya teknolojia ya Marekani ikiwa ni pamoja na Apple, Google na Meta yamefuta nyadhifa zenye jukumu la kuwadhaminia ajira watu wa rangi na mbari tofauti, na mwaka huu yamewaachisha kazi makumi ya maelfu ya wafanyikazi weusi au wasio wazungu kwa ujumla.
Michael Austin, mshauri wa gavana wa zamani wa Jimbo la Kansas na mwanachama wa Project 21 (mtandao wa wahafidhina weusi) anasema kuhusu suala hili kwamba: Mwaka huu, tumeona wafanyakazi zaidi wakifukuzwa, na Wamarekani weusi walikuwa na kiwango cha juu zaidi cha kutimuliwa kazi kuliko wafanyakazi wengine kwa asilimia 64.
Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa kwa pamoja wa gazeti la Marekani la Washington Post na taasisi ya utafiti wa maoni ya Ipsos yanaonyesha kuwa, asilimia 51 ya raia weusi wa Marekani hawana matumaini ya kuboreka hali ya ubaguzi wa rangi nchini humo, na idadi kubwa ya watu weusi walioshirikishwa katika utafiti huo wamesema hali ya ubaguzi wa rangi nchini Marekani itabaki kama ilivyo.
Pia, karibu 70% ya washiriki katika utafiti huu, ambao wana umri wa kati ya miaka 50 na 64, wanaamini kuwa hali ya sasa ya maisha ya vijana na barobaro weusi wa Marekani ni hatari zaidi kuliko siku za nyuma, na 60% ya watu wazima weusi wana wasiwasi kwamba, wao wenyewe au mmoja wa jamaa zao atashambuliwa na raia wazungu wa Marekani kwa sababu ya rangi yake nyeusi.
Kwa upande wa elimu, tovuti ya habari ya Marekani, Vox imeandika kuwa: Watoto weusi wanakabiliwa na uwezekano kubaguziliwa mashuleni mara tano zaidi ya wanafunzi wa kizungu.
Vilevile ubaguzi wa rangi umetajwa kuwa moja ya sababu muhimu za vifo vya akina mama wajawazito weusi huko Marekani, kwa kadiri kwamba Umoja wa Mataifa umetangaza katika muktadha huu kuwa, kiwango kikubwa cha vifo vya wajawazito kati ya wanawake weusi huko Amerika Kaskazini kinatokana na ubaguzi wa rangi kwa njia ya unyanyasaji wa kimaneno na kimwili wa watoa huduma za afya, pamoja na kunyimwa huduma bora na dawa za kutuliza maumivu.
Hali hii haishuhudiwi nchini Marekani pekee, bali ripoti zilizochapishwa kutoka Canada pia zinaonyesha kuwa wanawake, hata katika kazi za kitaaluma, mara nyingi hulalamika kuhusu unyanyasaji wa maneno, kupapaswa bila ya hiari yao, na mienendo ya ukatili na matusi kwenye maeneo ya kazi.
Pia, wanawake katika kazi za kitaaluma, kwa wastani, hupokea chini ya nusu ya mshahara wa wanaume katika kazi hizo hizo.
Kwa mujibu wa utafiti mpya uliofanywa na shirika la hisani la Kiislamu, Islamic Relief, zaidi ya theluthi mbili ya Waislamu wa Canada wanasumbuliwa na ubaguzi katika maeneo yao ya kazi. Waislamu hawa wamekumbana na ubaguzi rasmi, unaojumuisha ukosefu wa sawa katika kupandishwa vyeo, dhulma katika mishahara na majukumu ya kikazi, au sera za kibaguzi kama vile kanuni zinazohusiana na mavazi.
Huko barani ulaya pia, kuendelea na kushadidi sera za ubaguzi wa rangi na ubaguzi kumekuwa mgogoro mkubwa wa kisiasa na kijamii kiasi kwamba, katika miezi ya karibuni kumeshuhudiwa maandamano ya migomo mingi katika nchi kama Ujerumani na Ufaransa ikitaka kukomeshwa sera hizo za kibaguzi.