Russia: Shambulio la droni la Ukraine ni ugaidi wa kimataifa
Russia imelitaja shambulio la ndege zisizo na rubani (droni) za Ukraine dhidi ya Moscow kuwa ugaidi wa kimataifa.
Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesisitiza kuwa, jaribio la shambulio hilo la droni la Ukraine la mapema leo Jumatatu kusini mwa Moscow limetibuliwa na vikosi vya usalama vya Russia.
Amesema, "Shambulio la kigaidi kwa kutumia droni mbili dhidi ya Moscow limetibuliwa kwa kutumia mifumo ya vita vya kielektroniki (ya Russia)."
Zakharova amenukuliwa na shirika la habari la TASS akisema kuwa, majengo kadhaa ambayo sio ya makazi ya watu yameharibiwa kwenye shambulio hilo la Kiev kwa kutumia droni mbili.
Kwa mara nyingine tena, Zakharova amezishutumu nchi za Magharibi kwa kuchochea moto wa vita vya zaidi ya mwaka mmoja nchini Ukraine ambavyo vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu.
Aidha Wizara ya Ulinzi ya Russia imetangaza habari ya kuzimwa kwa shambulio hilo la droni, na kusisitiza kuwa hakuna mtu yoyote aliyepoteza maisha au kujeruhiwa kwenye tukio hilo.
Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa, ndege 11 zisizo na rubani za Ukraine zimetunguliwa kwa kutumia mifumo ya ulinzi wa anga ya Russia katika eneo la Crimea, ambayo ni sehemu ya ardhi ya shirikisho la Russia.
Tangu vilipoanza vita kati ya Russia na Ukraine, nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zimefanya juhudi kubwa kupindukia kujaribu kuzuia kupata ushindi Russia katika vita hivyo. Hadi hivi sasa zimeshatumia makumi ya mabilioni ya dola kuisheheneza Ukraine silaha za kila namna.