Moscow yawaonya magaidi wasijaribu kushambulia wanajeshi wa Russia na Syria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i100648-moscow_yawaonya_magaidi_wasijaribu_kushambulia_wanajeshi_wa_russia_na_syria
Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema kuwa, Moscow ina taarifa kwamba magenge ya kigaidi yanapanga njama za kutumia magaidi wa kujiripua kwa mabomu dhidi ya wanajeshi wa Russia na Syria na kwamba inatoa onyo mapema kuhusu njama hizo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 04, 2023 02:34 UTC
  • Moscow yawaonya magaidi wasijaribu kushambulia wanajeshi wa Russia na Syria

Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema kuwa, Moscow ina taarifa kwamba magenge ya kigaidi yanapanga njama za kutumia magaidi wa kujiripua kwa mabomu dhidi ya wanajeshi wa Russia na Syria na kwamba inatoa onyo mapema kuhusu njama hizo.

Genge la kigaidi la Jabhat al Nusra ambalo limekuwa likipata pigo mfululizo kutoka kwa wanajeshi wa Syria na wapambanaji wa kambi ya muqawama katika maeneo tofauti ya nchi hiyo, limekuwa likifanya njama za kigaidi mara kwa mara dhidi ya taifa hilo la Kiarabu walilolivamia.

Shirika la habari la Sputnik limemnukuu Admirali Vadim Kulit, Naibu wa Mkuu wa Kituo cha Wizara ya Ulinzi ya Russia cha Kuleta Mapatano baina ya Pande Hasimu nchini Syria akisema kuwa, Russia ina wasiwasi sana na taarifa zinazoonesha kuwa magaidi wa Jabhat al Nusra wanapanga njama za kuendesha mashambulio ya kujiripua kwa mabomu dhidi ya wanajeshi wa Russia na Syria hasa kwenye misafara ya doria ya wanajeshi wa nchi hizo mbili.

Syria imetumbukizwa kwenye vita angamizi kwa msimamo wake wa kutokubali kuburuzwa na madola ya kibeberu

 

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Russia amesema, jeshi la nchi hiyo huko Syria litachukua hatua kali sana dhidi ya genge la Jabhat al Nusra iwapo litafanya mashambulio kama hayo.

Vile vile amewataka makamanda wa genge hilo la kigaidi wasijaribu kufanya chokochoko zozote na waendelee kuheshimu makubaliano ya kupunguza hali ya wasiwasi vinginevyo watakumbwa na majibu wasiyoyatarajia.

Hivi karibuni Russia na Syria ziliendesha operesheni za pamoja za anga na mizinga za kuendelea kukomboa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na utawala wa Kizayuni wa Israel, Marekani na Uturuki na operesheni hizo zimefanyika kwa mafanikio makubwa.