Aug 09, 2023 11:26 UTC
  • Russia: Marekani ndiyo ya kulaumiwa kwa kutotekelezwa JCPOA

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema mustakabali wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA upo mikononi mwa Marekani na nchi za Ulaya, huku akitilia shaka azma ya Wamagharibi ya kuyahuisha mapatano hayo kikamilifu.

Sergei Ryabkov amesema hayo katika kikao na waandishi wa habari hapa mjini Tehran na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza ahadi na majukumu yake bila ya dosari au ukiukaji wowote baada ya kusaini mapatano hayo ya JCPOA mwaka 2015 kwa lengo la kuondolewa vikwazo vya kidhalimu vya Washington.

Suala la Iran kufungamana na majukumu yake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA limethibitishwa katika ripoti 16 za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). 

Ryabkov ameeleza bayana kuwa, Marekani ndiyo inayopaswa kubeba dhima ya changamoto za utekelezaji zinayokabili mapatano hayo ya dunia ambayo Washington ilijiondoa kwayo mwaka 2018.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia kukutana na wenzake wa Iran, Ali Bagheri-Kani na Reza Najafi hapa Tehran imesema: Tehran na Moscow zinaamini kuwa, kutotekelezwa kikamilifu makubaliano ya JCPOA kumetokana na sera ghalati ya Marekani ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran.

Iran na Russia zimesisitiza kuwa, JCPOA ndiyo mapatano bora zaidi na hakuna mbadala wake. Msimamo huu wa Iran na Russia unafanana na uliotolewa karibuni na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ambaye alisema katika ripoti yake ya 15 kuhusu azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la umoja huo kwamba: Mapatano ya JCPOA bado ni chaguo bora.

Tags