Sep 15, 2023 11:50 UTC
  • Ripoti: Karibu robo milioni ya watu wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula

Takriban watu milioni 238 wanasumbuliwa na viwango vya juu vya ukosefu wa usalama (utoshelevu) wa chakula katika nchi 48 duniani.

Hayo yamesemwa kwenye Ripoti ya Ulimwengu Kuhusu Migogoro ya Chakula ya mwaka huu 2023 iliyoeleza kuwa, nchi nne miongoni mwazo zinakabiliwa na hali mbaya zaidi ya kutisha ya ukosefu na uhaba wa chakula.

Ripoti hiyo iliyotolewa jana Alkhamisi imeeleza kuwa, watu milioni 33.64 wanakabiliwa na 'hali za dharura' katika nchi 36 duniani, huku wengine 128,600 wakisumbuliwa na 'hali za maangamivu' katika nchi nne duniani.

Ripoti hiyo imesema Sudan Kusini ndiyo ina kiwango kikubwa zaidi cha ukosefu wa usalama wa chakula kwa asilimia 63, ikifuatiwa na Yemen iliyosajili kati ya asilimia 52 na 55 katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu. 

Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Haiti na Sudan kila moja inakabiliwa na ukosefu wa chakula kwa asilimia 40, sawa na kiwango cha tatu au zaidi cha vigezo vya kimataifa vya usalama wa chakula duniani.

Takwimu za Shirika la Mpango wa Chakula Duniani zinaonesha kuwa, watu zaidi ya milioni 20 katika Pembe ya Afrika wanakabiliwa na viwango vya kutisha vya uhaba wa chakula. Aidha karibu watu milioni 43 wanakabiliwa na uhaba wa chakula Afrika Magharibi, mara nne zaidi ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita.

Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres alisema zaidi ya watu milioni 780 wanateseka kwa njaa kote ulimwenguni na hawajui watatoa wapi mlo ujao; lakini wakati huo huo karibu theluthi moja ya chakula ulimwenguni kinaharibiwa au kupotea.  

Tags