Mabadilishano ya wafungwa na kuendelea misimamo ya Marekani dhidi ya Iran
(last modified Wed, 20 Sep 2023 02:37:30 GMT )
Sep 20, 2023 02:37 UTC
  • Mabadilishano ya wafungwa na kuendelea misimamo ya Marekani dhidi ya Iran

Kufuatia mafanikio ya kubadilishana wafungwa kati ya Iran na Marekani Jumatatu ya juzi, raia watano wa Iran ambao walifunguliwa mashtaka kinyume cha sheria na vyombo vya mahakama vya Marekani kutokana na shughuli za kawaida za kibiashara waliachiliwa huru.

Aidha takriban dola bilioni 6 za mali za Iran ambazo zilikuwa zimezuiwa kinyume cha sheria nchini Korea Kusini zilihamishiwa katika akaunti za Iran huko Qatar.

Kadhalika katika fremu ya makubaliano kati ya Iran na Marekani, ambayo ni matokeo ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja, raia 5 wenye uraia pacha wa Iran na Marekani waliokuwa wamefungwa jela nchini Iran kwa sababu za kijasusi na kiusalama waliachiwa huru na kuhamishiwa nchini Qatar.

Baada ya kutekelezwa mabadilishano hayo, maafisa wakuu wa Marekani walichukua msimamo dhidi ya Iran na kutoa tuhuma za uwongo dhidi ya taifa hili. Miongoni mwao ni Rais Joe Biden wa nchi hiyo ambaye huku akithibitisha kuachiliwa kwa wafungwa wa Kimarekani nchini Iran, alitangaza kuwawekea vikwazo Rais wa zamani wa Iran Mahmoud Ahmadinejad na Wizara ya Kiintelijensia ya Jamhuri ya Kiislamu.

Sambamba na hilo, aliwataka Wamarekani wajizuie kusafiri kwenda Iran. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani Anthony Blinken sambamba na kusisitiza juu ya ulazima wa Wamarekani kutosafiri kwenda Iran, alikariri tuhuma za hapo awali kuhusu kile alichokiita kuwa eti "utekaji nyara raia wa Marekani unaofanywa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran" kwa ajili ya malengo ya kisiasa na kiuchumi.

 

Nukta muhimu ni kwamba, licha ya anga ya kipropaganda na makelele yaliyoibuliwa na mamlaka za Marekani sambamba na maonyo makali kuhusu kutosafiri kwenda Iran, ukweli ni kwamba kwa kutilia maanani maisha ya mamia ya maelfu ya Wairani nchini Marekani, idadi kubwa sana miongoni mwao huzuru nchi yao na kutembelea jamaa zao kila mwaka tena bila ya vizingiti na mibinyo yoyote na kurejea Marekani bila tatizo. Kwa msingi huo madai dhidi ya Iran ya maafisa wa utawala wa Biden hayaoani na ukweli na uhalisia wa mambo.

Sanjari na hayo, Wamarekani wengi wamesafiri kuja Iran bila matatizo yoyote kutokana na vivutio vyake vya kiutamaduni, kihistoria na kimaumbile, na wamesifu muamala mzuri wa Wairani na hasa ukarimu na moyo wao wa kuingiliana na watu.

Kadhia ya pili iliyoibuliwa na maafisa wa Marekani katika fremu ya makubaliano yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, ingawa zaidi ni kwa lengo la kujibu ukosoaji wa ndani, hususan kutoka kwa Warepublican, ni jinsi ya kutumia mali iliyotolewa na Iran kutoka Korea Kusini, ambayo sasa imehamishiwa katika benki za Qatari. Maafisa wa Marekani wamekuwa wakizungumza mara kwa mara kuhusu kudhibiti, kusimamia na kufuatilia vyanzo vya hivi vya fedha na uwezekano wa kuvizuia tena.

John Kirby

 

Miongoni mwao ni John Kirby, mratibu wa kistratejia wa Baraza la Usalama la Taifa la Marekani amedai kuwa, iwapo Iran itatumia fedha hizo zilizoachiliwa kwa malengo yasiyo ya kibinadamu, Washington inaweza kuzuia kukabidhiwa fedha kwa serikali ya Tehran. Inaonekana kuwa, misimamo kama hii ina matumizi ya ndani zaidi na inatolewa na maafisa wa serikali ya Biden kujibu shutuma za wapinzani wao kuhusu makubaliano hayo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani.

Hata hivyo, maafisa wakuu wa Iran wamepinga vikali madai hayo na kusisitiza kuwa, serikali ya Iran itazitumia fedha hizo kwa njia yoyote inayoona inafaa na hakuna mtu au dola lenye mamlaka ya kuiainishia namna ya kutumia fedha hizo.

Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaamua jinsi ya kutumia dola bilioni 6 ambazo ni fedha zake zilizokuwa zinazuiliwa Korea Kusini. Amesema fedha hizo ambazo zimeachiliwa kama sehemu ya mchakato wa kubadilishana wafungwa na Marekan "zitatumika popote zitakapohitajika".

Nukta ya mwisho ni kwamba licha ya makubaliano ya hivi karibuni na Iran, lakini serikali ya Biden imeendelea kupiga ngoma ya uadui dhidi ya taifa hili la Kiislamu na kusisitiza msimamo wake wa chuki dhidi ya Iran na msisitizo wake wa kukabiliana na Tehran.

Rais Ebrahim Raisi

 

John Kirby, mratibu wa kistratijia wa Baraza la Usalama la Taifa la Marekani anasema kuhusiana na hili kwamba: Makubaliano ya kubadilishana wafungwa na Iran hayamaanishi mabadiliko katika siasa za Washington dhidi ya Iran, na kwamba, utendaji wa kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu unaendelea katika eneo na ulimwengu kwa ujumla.

Kusimama kidete Tehran katika misimamo yake katika makubaliano yasiyo ya moja kwa moja ya hivi karibuni na Marekani kuhusu kuachiliwa huru wafungwa wake na mali zilizozuiwa ni ushindi mwingine dhidi ya Marekani. Hasa kwa kuzingatia kwamba, Iran ilionyesha msimamo thabiti mbele ya madai ya Washington ya kuachiliwa huru wafungwa wenye uraia wa nchi mbili kwamba, sharti la kutimia hilo ni kuachiliwa na kuhamiishwa kikamilifu fedha zake zilizokuwa zimezuiwa na kwa utaratibu huo ikawa imeonyesha kutoiamini hata chembe Marekani kutokana na ukiukwaji wa mara kwa mara wa ahadi za zake.