Ufaransa yakumbwa na maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi
(last modified 2023-09-25T04:59:10+00:00 )
Sep 25, 2023 04:59 UTC

Maelfu ya wananchi wa Ufaransa jana Jumapili waliandamana katika mitaa mbalimbali ya mji mkuu Paris na katika miji mingine nchini humo wakilalamikia ubaguzi wa rangi wa kimfumo unaoendelea kushuhudiwa nchini humo.

Waandamanaji wametangaza kuanza msimu mpya wa maandamano na kusema watasitisha maandamano hayo iwapo tu matakwa yao dhidi ya kile kinachojulikana kama "ubaguzi wa rangi wa kimfumo, ukandamizaji wa polisi na ukosefu wa uadilifu wa kijamii" yatakidhiwa kikamilifu.  

Ubaguzi wa rangi umekuwa tatizo kubwa kwa Wazungu. Kuenea kwa ubaguzi wa rangi katika nchi mbalimbali za Ulaya ikiwa ni pamoja na Ufaransa, Uingereza na Ujerumani, kumechochea na kushadidisha malalamiko na kutoridhishwa wananchi katika nchi hizo katika miezi ya hivi karibuni. 

Suala hili, pamoja na kushadidi matatizo ya kiuchumi na kutoridhika wananchi na sera zinazotekelezwa na serikali hizo yemepelekea baadhi ya nchi za Ulaya kama Ufaransa kukabiliwa na mgogoro. 

Sheria za nchi nyingi za Ulaya ikiwa ni pamoja na nchi ya Ufaransa zinaeleza kuwa, hakuna mtu aliye na haki ya kuwanyima wengine haki zao za kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa sababu ya rangi ya ngozi zao, dini, umri au hali zao za ulemavu. Lakini ukweli wa mambo ni kuwa sheria hizi tajwa zimesalia kwenye karatasi tu bila kutekelezwa kivitendo katika nchi za Magharibi.

Tags