Maelfu waandamana Ujerumani kupinga kupewa silaha Ukraine
Maelfu ya watu wamefanya maandamano katika mji wa Munich, kusini mwa Ujerumani kupinga vita na kupewa silaha Ukraine.
Vyombo vya habari vya Ujerumani vimeripoti kuwa, maandamano hayo yamefanyika chini ya kaulimbiu ya "Munich Inasimama na Uhuru Bila Silaha."
Waandamanaji hao waliokusanyika katika Medani ya Marienplatz mjini Munich wakati nchi hiyo ya Ulaya ikiadhimisha duru ya 33 ya Siku ya Umoja, wametoa mwito wa kusitishwa vita vya Ukraine, sambamba na kuanza mazungumzo ya amani.
Kadhalika waandamanaji hao wameitaka serikali ya Ujerumani ijiondoe katika Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO).
Miongoni mwa shakhsia maarufu walioshiriki na kutoa hotuba kwenye maandamano hayo ni mwanasiasa Jurgen Todenhofer na mwandishi wa vitabu Markus Krall .
Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zimeendelea kurundika na kuimiminia silaha Ukraine zikiwemo hata zilizopigwa marufuku kimataifa.
Ujerumani imeipa Ukraine silaha na zana nyingi za kijeshi zenye thamani ya mabilioni ya Yuro, vikwemo vifaru vya kisasa kabisa aina ya Leopard 2.
Vita vya Ukraine vinatajwa kuwa ni fursa ya kufanyia majaribio silaha za kisasa na kutumiwa silaha za zamani za nchi nyingi za Ulaya za Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO ikiwemo Ujerumani.