Chuki dhidi ya wahajiri Uingereza zaongezeka baada ya Brexit
https://parstoday.ir/sw/news/world-i10357-chuki_dhidi_ya_wahajiri_uingereza_zaongezeka_baada_ya_brexit
Chuki dhidi ya wahajiri nchini Uingereza zimeongezeka kwa asilimia 500, siku chache baada ya nchi hiyo kupiga kura ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 01, 2016 03:39 UTC
  • Chuki dhidi ya wahajiri Uingereza zaongezeka baada ya Brexit

Chuki dhidi ya wahajiri nchini Uingereza zimeongezeka kwa asilimia 500, siku chache baada ya nchi hiyo kupiga kura ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit.

Baraza la Taifa la Polisi Uingereza (NPCC) limesema katika kipindi cha wiki moja iliyopita tangu nchi hiyo ijitoe EU, limerekodi kesi 330 zinazohusu jinai za chuki haswa dhidi ya wahajiri, ikilinganishwa na wastani wa kesi 63 kwa wiki hapo awali. Sara Thornton, mkuu wa baraza hilo amesema wameshangazwa sana na ongezeko hilo la chuki dhidi ya wahamiaji na hawaelewi lina mafungamano gani na hatua ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya. Amesema kuwa baadhi ya jinai wanazofanyiwa wahajiri nchini humo ni pamoja na kupigwa, kutukanwa, kurushiwa vijikaratasi vyenye jumbe za kuwadhalilisha na kukejeliwa katika mitandao ya kijamii.

Haya yanajiri katika hali ambayo, chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Uingereza pia imeripotiwa kuongezeka maradufu katika miezi ya hivi karibuni. Baraza la Waislamu nchini humo limesema kuwa, mwishoni mwa wiki iliyopita pekee, walinakili kesi 100 za jinai za chuki dhidi ya Waislamu kote nchini. Dakta Shuja Shafi, Katibu Mkuu wa baraza hilo amesema wamerekodi ongezeko la asilimia 70 ya jinai zinazotokana na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu katika mji wa London pekee, katika muda wa mwaka mmoja uliopita.