Waziri Mkuu wa Uhispania: Israel haiheshimu sheria za kimataifa za ubinadamu
Waziri Mkuu wa Uhispania amesema kwamba, kwa kuzingatia idadi ya raia wakiwemo watoto wadogo ambao ni wahanga wa vita vya wiki kadhaa vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza, ni wazi kuwa Tel Aviv haiheshimu sheria za kimataifa za ubinadamu.
Pedro Sanchez, Waziri Mkuu wa Uhispania alisema hayo jana Alkhamisi katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya serikali ya TVE na kusisitiza kuwa, uvamizi wa kijeshi wa Israel dhidi ya Gaza ni jambo lisilokubalika hata kidogo.
Ameeleza bayana kuwa, "Kanda za video tunazoona, na ongezeko la idadi ya watoto wanaouawa, nina mashaka makubwa (Israel) inafungamana na sheria za kimataifa za ubinadamu."
Sanchez ameeleza bayana kuwa, "Wakati umefika sasa kwa jamii ya kimataifa hasa Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wa umoja huo kuitambua nchi ya Palestina."
Ameeleza kuwa, hatua ya EU kuitambua Palestina itahitimisha mgogoro baina ya utawala haramu wa Israel na Palestina, na vile vile italeta uthabiti katika eneo la Asia Magharibi.
Waziri Mkuu wa Uhispania amesisitiza kuwa Madrid ipo tayari kuitambua rasmi kwa upande mmoja nchi ya Palestina hata kama hatua hiyo itapingana na mtazamo wa Umoja wa Ulaya. "Tunachoshuhudia Gaza hakikubaliki," ameongeza Waziri Mkuu wa Uhispania.
Wiki iliyopita, hatua ya Uhispania na Ubelgiji ya kutangaza kuwa tayari kuitambua rasmi nchi huru ya Palestina mbali na kuwa tukio muhimu kushuhudiwa barani Ulaya kuhusu kadhia ya Palestina, lakini pia iliukasirisha utawala wa Kizayuni.