Rais Erdogan wa Uturuki: Hakuna tofauti kati ya Hitler na Netanyahu
(last modified Thu, 28 Dec 2023 06:45:58 GMT )
Dec 28, 2023 06:45 UTC
  • Rais Erdogan wa Uturuki: Hakuna tofauti kati ya Hitler na Netanyahu

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema, "hakuna tofauti" kati ya kile waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu anakifanya katika mashambulizi ya miezi kadhaa sasa huko Gaza na kile kiongozi wa Nazi Adolf Hitler alikifanya miongo kadhaa iliyopita.

Akihutubia jana Jumatano katika hafla ya utoaji tuzo ya sayansi iliyofanyika mjini Ankara, Erdogan alimhutubu Netanyahu kwa kumuuliza: "hivi wewe (Netanyahu) unatofautianaje na Hitler? Watatufanya tufikirie kuwa uovu wa Hitler ni mdogo zaidi. Lakini je, kuna chochote anachofanya Netanyahu ambacho ni kidogo kuliko Hitler? Hapana."

Rais wa Uturuki amelinganisha jinsi wanavyotendewa duniani kote wasomi wanaothubutu kukemea ukandamizaji na mateso yanayofanywa leo na yaliyofanywa katika Ujerumani ya Nazi miaka 80 iliyopita.

"Kugeuzwa mbuzi wa kafara" kumeanzishwa dhidi ya mtu yeyote anayeikosoa Israel, ikiwa ni pamoja na wanachuo katika taasisi nyingi za kimataifa za elimu", amesema Erdogan.

Amebainisha kuwa wasomi nchini Marekani na kwingineko wanafukuzwa kazi au kulaumiwa kwa kuwatetea Wapalestina, na pia kukabiliwa na mashinikizo na vitisho, sawa na wale waliowatetea Wayahudi miongo kadhaa iliyopita.

Katika hotuba yake hiyo, rais wa Uturuki ameeleza kuwa, kuanzia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hadi mashirika ya habari, Umoja wa Ulaya mpaka makundi ya waandishi wa habari pamoja na asasi zote zinazotumika kama vinara wa demokrasia, zimefeli katika kukabiliana na mashambulio ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Gaza.

Ameendelea kueleza kwamba, si mashirika ya kimataifa pekee, lakini hata vyuo vikuu vinavyotajika vya Magharibi vimefeli katika mtihani wa suala la Gaza.

Marais wa vyuo vikuu vitatu mashuhuri vya Marekani waliowekwa 'kitimoto' na bunge la nchi hiyo kwa sababu ya utawala wa Kizayuni wa Israel 

"Hivi unaweza kufikiria marais wa vyuo vikuu wanahojiwa na kuwajibishwa katika Kongresi kwa sababu tu wanatetea haki za watoto, wanawake na raia?" amehoji Erdogan, akimaanisha marais wa vyuo vikuu vya Harvard, Pennsylvania na MIT, ambao mnamo Desemba 5 walifikishwa mbele ya bunge la Marekani ili kusailiwa kuhusiana na tuhuma za kuwepo uenezaji chuki dhidi ya Uyahudi kwenye vyuo vikuu hivyo.

Rais wa Uturuki amesema, ukosoaji mdogo kabisa unaofanywa hata ndani ya mipaka ya sheria na demokrasia unakandamizwa kwa kibandikwa chapa ya chuki dhidi ya Wayahudi, na unachukuliwa kuwa ni kosa la jinai.

Aidha amekiri kuwa, licha ya juhudi za kidiplomasia zilizofanywa na nchi zenye dhamiri kama Uturuki, kwa bahati mbaya, imeshindikana hadi sasa kuzuia mauaji ya mamia ya watu wanaouawa kila siku huko Ukanda wa Gaza.

Duru rasmi za Palestina zimetangaza kuwa, hadi sasa Wapalestina zaidi ya 21,000 wameuawa shahidi kutokana na mashambulio ya kinyama yanayoendelea kufanywa na jeshi la kigaidi la utawala dhalimu wa Kizayuni wa Israel.../