Jan 05, 2024 07:44 UTC
  • Beijing yaionya Taipei huku uchaguzi ukikaribia kufanyika katika kisiwa cha Taiwan

Huku uchaguzi mkuu wa rais na bunge ukikaribia kufanyika huko Taiwan tarehe 13 January, kiongozi wa ngazi ya juu ya China ameutaja uchaguzi huo kuwa chaguo kati ya vita na amani.

Uchaguzi wa rais na wabunge nchini Taiwan umepangwa kufanyika Januari 13, huku uhusiano kati ya Taipei na Beijing ukiwa umeharibika kwa kiwango ambacho kilikuwa hakijawahi kushuhudia tena katika miaka ya hivi karibuni. Taiwan ni kisiwa chenye utawala wa ndani ambacho China inakichukulia kuwa sehemu ya ardhi yake na kuwa shambulio la kijeshi litakuwa chaguo la mwisho katika juhudi za kukiunganisha na ardhi mama. Ni kuhusiana na jambo hilo ndipo, katika miezi ya hivi karibuni, China ikawa inafanya mazoezi ya kijeshi ya mara kwa mara katika eneo hilo ili kutoa mashinikizo na kuthibitisha madai ya umiliki wa kisiwa hicho. Ni kwa sababu hiyo ndio China katika kipindi cha wiki za hivi karibuni ikiwa inautaja uchaguzi ujao wa Taiwan kuwa chaguo kati ya vita na amani.

Bendera za China na Taiwan

Katika onyo la hivi karibuni la China kwa Taiwan, Zhang Zhijun, Mkuu wa Jumuiya ya Mahusiano ya Lango la Taiwan na mkuu wa Ofisi ya Masuala ya Taiwan katika miaka ya 2013 hadi 2018, akaashiria Jumatano matokeo mabaya ya kufanyika uchaguzi nchini Taiwan na akawataka watu wa eneo hilo kuwa makini katika uchaguzi huo. Ameuelezea uchaguzi huo kama chaguo baina ya vita na amani ua ustawi na kuporomoka. Zhang ameongeza kuwa, uzalendo wa Taiwan unapaswa kujengeka juu ya historia na chaguo sahihi ili kukuza uhusiano na kukirejesha kisiwa hicho kwenye njia sahihi ya maendeleo na amani.

Rais Xi Jinping wa China katika hotuba yake aliyotoa siku ya Jumapili katika maadhimisho ya mwaka mpya, alisema kuwa kuunganishwa kisiwa cha Taiwan na China ni jambo la dharura, na kusisitiza kwamba kurejeshwa umoja na nchi mama ni jambo lisiloepukika. Xi Jinping aliongeza kuwa, wananchi wa pande zote za Lango-Bahari la Taiwan wanapasa kuungana chini ya lengo moja na kujitahidi kuboresha ustawi wa taifa la China moja.

Mashinikizo mapya ya China dhidi ya Taiwan yanatolewa katika hali ambayo uchaguzi wa rais na bunge la eneo hilo unakaribia kufanyika, huku Beijing ikikerwa na chama tawala cha Taiwan cha Democratic Progressive Party na mgombea wake wa urais, Lai Ching-te, ambaye ana nafasi ya juu zaidi ya kushinda uchaguzi huo na ambaye China inaamini kuwa ana mielekeo ya kujitenga. Lai Ching-te, makamu wa rais wa sasa na ambaye ni mgombea urais wa chama tawala cha Taiwan cha Democratic Progressive Party (DPP), amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba hana mpango wa kubadilisha jina rasmi la kisiwa hicho, yaani "Jamhuri ya China", na kwamba ni watu wa Taiwan pekee ndio wanaoweza kuchukua uamuzi juu ya mustakbali wao.

 Tsai Ing-wen, rais wa eneo la Taiwan, ambaye anaungwa mkonona nchi za Magharibi, anasema kuwa uhusiano wa kisiwa hicho na China utaamuliwa tu na wananchi na kwamba makubaliano ya amani ya aina yoyote yanapaswa kujengeka juu ya misingi ya utu na kuheshimiana pande mbili. Ing Wen anaamini kuwa China inapasa kuheshimu matokeo ya uchaguzi ujao wa Taiwan na kwamba pande zote mbili zina jukumu la kudumisha amani na utulivu katika Lango-Bahari la Taiwan. Taiwan imekuwa ikiituhumu China  kuwa inajaribu kuvuruga matokeo ya uchaguzi wa kisiwa hicho kwa kueneza habari bandia au kutoa mashinikizo ya kibiashara na kijeshi. Hata hivyo, maafisa wakuu wa China wanasisitiza kwamba Taiwan iko katika hali mgumu na kwamba kuchukuliwa hatua yoyote ya kutaka kujitenga kutamaanisha vita.

Nancy Pelosi alipotembelea Taiwan

Kwa hakika, China katika miaka ya hivi karibuni imeeleza wasiwasi wake kuhusu harakati za kutaka kujitenga kisiwa kinachojitawala cha Taiwan, na kutahadharisha kuhusu juhudi zinazofanywa na Taipei za kukuza uhusiano wa kidiplomasia na nchi nyingine ikisema kuwa suala hilo ni chanzo cha mvutano. Kama ambavyo safari ya Nancy Pelosi, Spika wa Bunge la Wawakilishi la Marekani huko Taiwan mwaka 2022 iliongeza mvutano kati ya Beijing na nchi za Magharibi na kuilazimu China kufanya mazoezi makubwa ya kijeshi kukizunguka kisiwa hicho. Aidha, mwaka jana, kikao kilichofanyika kati ya Rais wa Taiwan na Kevin McCarthy, Spika wa Bunge la Wawakilishi la Marekani aliyeondolewa madarakani, huko California, kiliamsha hasira ya China na kuipelekea kufanya mazoezi ya kijeshi ya siku tatu karibu na kisiwa cha Taiwan. Kwa upande mwingine, hatua za kijeshi za China kandokando mwa  kisiwa hicho zimezifanya nchi za Magharibi kutoa jibu ambapo Rais Joe Biden wa Marekani amesema kwamba kukitokea vita, atatuma wanajeshi wa Marekani katika eneo hilo ili kuilinda Taiwan. Katika kumjibu, Rais wa China ameitaka Marekani "kuheshimu mamlaka na umoja wa ardhi ya nchi hiyo" kwa mujibu wa makubaliano ya pande mbili.

 

Tags