Jan 19, 2024 03:27 UTC
  • Indhari ya Uhispania kuhusu matukio ya eneo na ya kimataifa ya vita vya Gaza

Pedro Sánchez, Waziri Mkuu wa Uhispania ameonya kuwa, usalama na uthabiti wa eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) umekuwa hatarini na kwamba, mashambulizi haya yanahatarisha nidhamu na uratibu wa ushirikiano wa pande kadhaa.

Waziri Mkuu wa Uhispania alisema hayo mjini Davos, Uswisi siku ya Jumatano. Sanchez amesisitiza kuwa: Mwenendo wa matukio ya hivi sasa hautawasaidia wananchi wa Palestina. Kilicho hatarini ni minyororo ya usalama, biashara, ustawi, utulivu wa Mashariki ya Kati nzima na kuendelea kwa nidhamu na uratibu wa pande nyingi.

Maafisa na viongozi waandamizi wa Uhispania hadi sasa wamechukua misimamo ya ukosoaji kuhusiana na vitendo vya jinai vya utawala wa Kizayuni. Miongoni mwao ni Waziri wa Haki za Kijamii wa Uhispania, Ione Belarra, hivi karibuni alisema: "Israel imeacha mamia ya maelfu ya watu (huko Gaza) bila umeme, maji, na chakula, na inawashambulia raia kwa mabomu, hatua ambayo ni adhabu ya pamoja na ukiukaji hatari wa sheria za kimataifa, na unaweza kuitwa kuwa ni “uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki.”

Waziri wa Haki za Kijamii wa Uhispania ameongeza kuwa, Umoja wa Ulaya na Marekani zinaihimiza Israel kuendeleza siasa zake za uhasama.

Jinsi Gaza inavyoshambuliwa na kuharibiwa na Israel

 

Indhari na onyo la Waziri Mkuu wa Uhispania kuhusu matokeo ya vita vya Gaza dhidi ya mwelekeo wa kieneo na kimataifa limetolewa kutokana na kuendelea mashambulizi ya anga na ardhini ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na mauaji ya kimbari ya wakaazi wa eneo hilo ambalo linahesabiwa kuwa moja ya maeneo yenye mrundikano zaidi wa watu duniani. Wizara ya Afya ya Gaza ilitangaza siku ya Jumatano Januari 17 kwamba, idadi ya mashahidi wa Kipalestina imefikia 24,448 na wengine 61,504 wamejeruhiwa.

Ukweli wa mambo ni kuwa, vita vya Gaza na sisitizo la utawala wa Kizayuni la kuendeleza mashambulizi yake ya jinai huko Gaza kwa kisingizio cha kujilinda, jambo ambalo bila shaka linatimia kwa uungaji mkono kamili na wa pande zote wa Marekani ikiwa ni mshirika wa kistratijia wa Israel na baadhi ya mataifa ya Ulaya kama Ujerumani na Uingereza, ni mambo ambayo yamekuwa taathira hasi na mbaya kwa utulivu, usalama na biashara ya kikanda na kimataifa.

Moja ya matokeo ya vita vya Gaza na taathira yake ya moja kwa moja kwa uchumi na biashara ya dunia ni hatua ya Yemen katika Bahari Nyekundu ya kuunga mkono Wapalestina na ombi la kukomesha mzingiro wa Gaza kwa kupora au kushambulia meli zinazoelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel).

Mashambulio ya Yemen dhidi ya meli za kibiashara zinazoelekea Israel au zenye uhusiano na utawala wa Kizayuni, ambapo pamoja na kusababisha uharibifu mkubwa kwa Israel ambayo zaidi ya asilimia 90 ya biashara yake ya nje inategemea bahari, wakati huo huo gharama za biashara ya baharini duniani (hasa kwa mataifa ya magharibi) pia imeongezeka kwa kiasi kikubwa.

Zaidi ya wanajeshi 500 wa Israel wameuawa tangu Israel ianzishe mashambulio dhidi ya Ukanda wa Gaza

 

Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Majini lilitangaza mapema mwanzoni mwa mwezi huu wa Januari kwamba, makampuni 18 makubwa ya meli duniani yalisema yamechagua njia ndefu ya kuzunguka Afrika kwa ajili ya usafiri wa meli zao kutokana na mashambulizi dhidi ya meli katika Bahari Nyekundu. Kwa muktadha huo, kushadidi hali ya usalama katika Bahari Nyekundu kumesababisha makampuni makubwa ya meli kusafiri kilomita 25,000 hadi katika masoko ya Asia na kuhamisha bidhaa zao kwa kuvuka Rasi ya Tumaini Jema (Cape of Good Hope).

Matokeo ya tatizo hili ni ongezeko la miezi miwili katika muda wa safari za kibiashara. Jambo hilo limesababisha makampuni na serikali mbalimbali kuishinikiza Marekani ili kuulazimisha utawala wa Kizayuni kuondoa mzingiro dhidi ya Gaza.

Matokeo mengine ya vita vya Gaza ni kuongezeka kwa machafuko na ukosefu wa utulivu na vita katika maeneo mengine ya Magharibi mwa Asia. Kadhalika, baada ya Marekani kushindwa kuunda muungano wa wanamaji dhidi ya Yemen katika Bahari Nyekundu, ikishirikiana na Uingereza mara kadhaa zimefanya mashambulizi ya anga na makombora huko Yemen.

Hatua hizi, sambamba na uungaji mkono wa pande zote kwa Israel, kiutendaji zimepanua wigo wa kukosekana kwa utulivu na kuongeza uwezekano wa vita vikubwa katika eneo hilo. Onyo la Waziri Mkuu wa Uhispania pia limetolewa kwa kuzingatia matokeo ya kuendelea mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Gaza katika ngazi ya kieneo na kimataifa hususan katika nyanja za kiusalama, kiuchumi na kibiashara.

Tags