Russia: Marekani inatumia vita vya Ukraine kama mradi wenye faida
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa Marekani inaona vita kati ya Russia na Ukraine kama "mradi wa faida" na kusema: Moscow iko tayari kwa mazungumzo na Ukraine kwa ajili ya kumaliza mzozo huo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov ameuambia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba: Misaada ya Magharibi kwa Kiev inatatiza juhudi za kutafuta suluhisho la amani kwa mgogoro wa Ukraine na kwamba Kiev inashambulia kwa makusudi malengo ya raia.
Lavrov amefananisha msimamo wa Marekani katika kutoa misaada ya kijeshi kwa Ukraine na mradi wa biashara wenye faida na kusema: Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken, amejikita zaidi kwenye suala la kuendelezwa misaada kwa Ukraine kama dhamana ya kuunda nafasi mpya za kazi nchini Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameongeza kuwa: "Msaada wa kifedha wa Washington kwa Kiev sio ufadhili wa vita, lakini ni mradi wa biashara wenye faida, na mfano wazi wa ukweli huu ni kukabidhiwa kwa ardhi ya "Black Earth" kwa mfanyabiashara wa Marekani, George Soros kwa ajili ya kutupa taka kutoka kwenye viwanda vya kemikali vya nchi za Magharibi.
Sergei Lavrov amesisitiza kuwa "Ukraine inauza baadhi ya silaha za Magharibi kwenye soko la magendo na ni vigumu kufikiria kwamba nchi za Magharibi hazijui suala hili."
Wakati huo huo, Mkuu wa Shirika la Intelijensia la Russia amesema, Marekani imeanza kuunda "serikali ya kikoloni" nchini Ukraine inayojumuisha wanasiasa wa ndani ambao wamekula kiapo cha utiifu kwa Washington.
Sergey Naryshkin amefafanua kuwa, serikali ya Marekani imemtaka Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskky "kuwafutilia mbali" makumi ya maafisa wa ngazi za juu, ambao Washington haiwaamini tena katika nyadhifa zao kwa visingizio mbalimbali.